Jan 18, 2020 12:43 UTC
  • Kambi ya jeshi la Marekani ya Ainul Asad nchini Iraq
    Kambi ya jeshi la Marekani ya Ainul Asad nchini Iraq

Katika jitihada zake za kutimiza ahadi ya kulipiza kisasi kikali dhidi ya Marekani kutokana na mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na nchi hiyo dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wana jihadi wenzake, Alfajii ya Jumatano tarehe 8 Januari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishambulia kambi kubwa zaidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ya Ainul Asad.

Awali Rais Donald Trump wa Marekani ilidai kwamba, shambulizi hilo la makombora ya balestiki la Iran halikusababisha hasara ya nafsi lakini sasa habari zaidi kuhusu kadhia hiyo zinaanza kufichuka hatua kwa hatua. Mtandao wa habari wa Defense One Ijumaa ya jana ulifichua kwamba, askari wasiopungua 11 wa Marekani walijeruhiwa katika shambulizi hilo la wamepelekwa katika nchi za Ujerumani na Kuwait kwa ajili ya matibabu. Ijumaa ya jana pia jeshi la Marekani lilikiri kuwa, wanajeshi 11 wa nchi hiyo wanapewa matibabu kutokana na madhara ya ubongo waliyopata kutokana na shambulizi la makombora ya Iran. Msemaji wa Jeshi la Marekani magharibi mwa Asia, Kanali Myles Caggins amesema askari waliopatwa na madhara ya ubongo wa Marekani wamepelekwa Landstuhl huko Ujerumani na kwenye hospitali ya kambi ya Arifjan nchini kuwait kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi wa kiafya. Amedai kuwa hakuna askari aliyeuliwa katika shambulizi la makombora ya Iran huko Ainul Asad. 

Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa, jeshi la Marekani na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, zimedai kuwa zimepata habari hiyo hivi karibuni! 

Ainul Asad

Katika siku kadhaa zilizopita Rais Donalds Trump wa Marekani, Waziri wa Ulinzi Mark Esper na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Marekani wamekuwa wakidai kuwa katika shambulizi la makombora ya Iran dhidi ya kambi ya Ainul Asad hakuuliwa wala kujeruhi askari yeyote. Trump amefanya jitihada kubwa za kulinda haiba ya Marekani ambayo kwa mara ya kwanza kabisa tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, kambi yake ya kijeshi imeshambuliwa na jeshi la nchi nyingine katika kipigo cha Ainul Asad na kudai kuwa, hakuna askari hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa. 

Sababu nyingine iliyomfanya Trump afiche hasara zilizosababishwa na shambulizi la makombora ya balestiki ya Iran huko Ainul Asad nchini Iraq ni kutaka kujiepusha na mpambano wa moja kwa moja na Iran, jambo ambalo lingekuwa na taathira mbaya sana kwa Washington na washirika wake wa kanda hii ya magharibi mwa Asia. Katika matamshi yake ya awali baada ya shambulizi hilo, Trump alijaribu kuonesha kuwa si jambo muhimu  na kudai kwamba, limesababisha hasara ndogo kwa kambi hiyo ya jeshi la Marekani. Matamshi hayo ya Trump yalionesha jinsi Marekani inavyoogopa kukutana uso kwa uso na Iran katika medani ya kijeshi hususan kwa kutilia maanani kwamba, awali alikuwa ametishia kuwa, iwapo Iran itajibu hujuma yoyote ya Marekani, Washington itashambulia vituo 52 tofauti ndani ya Iran. Donald Trump ambaye ni mashuhuri sana kwa kusema uongo sasa anakabiliwa na kashfa nyingine ya kulidanganya taifa la Marekani kuhusu hasara zilizosababishwa na mashambulizi ya makombora ya balestiki ya Iran dhidi ya kambi kubwa zaidi ya nchi hiyo nchini Iraq. 

Kambi ya jeshi la marekani ya Ainul Asad imesawazishwa na udongo...

Maafisa wengine wa masuala ya ulinzi na usalama wa Marekani kama Waziri wa Ulinzi,  Mark Esper pia wamekuwa wakikariri madai kwamba, hakuna askari hata mmoja wa nchi hiyo aliyepatwa na madhara katika shambulizi la makombora ya Iran huko Ainul Asad. Hata hivyo wiki moja baada ya mashambulizi hayo gazeti la Washington Post lilifichua kwamba, wanajeshi wawili waliuawa kwa kurushwa kutoka kwenye mnara wa kambi hiyo na kwamba makumi ya wanajeshi wengine walizimia na kopoteza fahamu.

Sasa vyombo mbalimbali vya habari hususan vya Marekani vimeanza kuvujisha taratibu habari zinazohusiana na mashambulizi hayo na hapana shaka kuwa, siku zijazo zitafichua mengi na mengi zaidi… Mpaka hapa habari hii iliyothibitishwa na Pentagon ya kujeruhiwa wanajeshi wasiopungua 11 wa Marekani katika shambulizi hilo peke yake inakadhibisha madai ya Rais Donald Trump aliyedai kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Hali ni shwari na hakuna hata askari mmoja aliyepatwa na madhara.. 

Wanajeshi wa Marekani wakishangazwa na uharibifu mkubwa wa makombora ya Iran... Ainul Asad

Kufichuliwa kwa habari hizi kumepokewa kwa hisia kali ndani na nje ya Marekani. Baadhi ya familia za askari wa Marekani walioko nchini Iraq wameviambia vyombo vya habari kama televisheni ya CNN kwamba, hazina mawasiliano na ndugu na watoto wao waliokuwa katika kambi ya jeshi la Marekani ya Ainul Asad. Suala hili linaonesha jinsi serikali ya Donald Trump inavyofanya juhudi za kulinda haiba yake kwa kuficha au kuchuja habari zote zinazohusiana na shambulizi kali la makombora ya Iran huko Ainul Asad.        

Tags

Maoni