Jan 19, 2020 03:27 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani, chanzo cha shari zote Asia Magharibi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani ndiyo chanzo cha vitendo vyote vya shari, migogoro na matatizo katika eneo hili la Asia Magharibi.

Akizungumza jana Jumamosi katika kikao cha Jopo la Kupambana na Migogoro katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, kusini mashariki mwa nchi, Rais Rouhani ameeleza bayana kuwa, "Wamarekani ndio chimbuko la kila aina ya shari katika eneo. Mliona namna walivyomuua mmoja wa Majenerali wetu ambaye alikuwa kamanda mkuu wa kampeni dhidi ya ugaidi."

Tarehe 3 Januari mwaka huu, jeshi la Marekani lilimuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq tena uraiani. 

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na kutekeleza wajibu wake kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015, lakini Marekani ambayo ni mzizi wa shari katika eneo iliyakiuka.

Rais Rouhania na wakaazi wa mkoa wa Sistan na Baluchistan walioathiriwa na mafuriko

Ameongeza kuwa, "Tizama walivyofanya katika nchi za eneo kama Yemen, Iraq, Syria, Lebanon, Afghanistan na Pakistan. Tizama namna walivyonyonya utajiri wote wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, na namna walivyoliunga mkono kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, "tupo katika mkondo sahihi na tutaendelea kufuata njia hiyo ya ustawi kwa izza na nguvu zetu zote. Hatutasita kuwadhaminia usalama watu wetu na kuafikia malengo yetu kama taifa. Kile ambacho ni cha shari kwa Iran leo hii, ni cha shari kwa dunia nzima."

 

Tags

Maoni