Jan 19, 2020 06:40 UTC
  • Mchango mkubwa wa Iran katika kuwasaidia wakimbizi na kupambana na mgogoro wa ukimbizi duniani

Karibu miaka 40 sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwenyeji wa kundi kubwa la wakimbizi hasa raia wa Afghanistan na hivi sasa Tehran imesema, iko tayari kuwafaidisha wengine kwa uzoefu wake katika suala hilo.

Ivo Freijsen, mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Wakimbizi nchini Iran alisema jana Jumamosi wakati alipoonana na Mahdi Mahmoudi, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya  Wageni na Wahajiri wa Kigeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran kwamba anaishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake mkubwa kwa wakimbizi.

Licha ya kwamba jamii ya kimataifa haiipi Iran misaada ya kutosha ya kuhudumia wakimbizi, lakini Tehran inatoa mchango mkubwa kimataifa katika kupambana na mgogoro wa ukimbizi. Pamoja na kuwepo matatizo mengi lakini miaka yote hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kupunguza juhudi zake za kuwahudumia wakimbizi. Miaka yote hii Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeshindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake kuhusu wakimbizi walioko Iran kiasi kwamba hadi hivi sasa inatoa asilimia 6 tu ya gharama za kuwahudumia wakimbizi wa Afghanistan humu nchini.

Ivo Freijsen

 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Abdolreza Rahmani Fazli naye alisema mwezi Januari 2019 wakati alipoonana na Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Wakimbizi mjini Geneva Uswisi kwamba hali ya eneo hili hivi sasa iko katika namna ambayo iwapo haitazingatiwa ipasavyo, basi tatizo la wakimbizi kamwe halitotauliwa. 

Ukimbizi mara zote huambatana na masuala kama ya madawa ya kulevya, ugaidi, uasherati, uhalifu, uchafuzi wa mazingira, kutoheshimu sheria na masuala mengine mengi mabaya, na kama mashirika ya kimataifa na nchi za dunia zitashindwa kutekeleza vilivyo majukumu yao, basi wimbi la wakimbizi na wahamiaji litakuwa kubwa kwenye.

Kwa upande wake, Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Wakimbizi ametilia mkazo matatizo yanayotokana na vikwazo vya upande mmoja na Marekani dhidi ya Iran na aidha amesema, hatua ambazo Umoja wa Mataifa umepanga kuzichukua ni ndogo sana ikilinganishwa na huduma zinazotolewa na Iran kwa wakimbizi. 

Abdolreza Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iran

 

Kwa kweli Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa huduma nyingi kwa wakimbizi wa Afghanistan. Miongoni mwa huduma hizo ni kutoa elimu kwa wakimbizi laki nne na 80 elfu, kuanzia chekechea hadi cheti, kuwapa haki ya kuwa na leseni ya udereva, kuwapa haki sawa katika vyombo vya mahakama, kupigwa chanjo sawa na raia wa Iran, kupewa nafasi katika vyuo vikuu ambapo hadi hivi sasa wakimbizi 16 elfu na 500 wametumia fursa hiyo ya kupata elimu ndani ya vyuo vikuu nchini Iran, kupewa huduma za bima ya afya na vile vile kupewa wakimbizi hao vitambulisho maalumu vya kuwaruhusu kufanya kazi nchini Iran. 

Vile vile kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, elimu kwa wakimbizi wa Afghanistan inatolewa bure, bila ya kujali wakimbizi hao wanaishi kihalali au kinyume cha sheria humu nchini.

Hiyo ni sehemu ndogo tu ya huduma nyingi zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakimbizi, licha ya kwamba mchango wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa ni asilimia sita tu kwa wakimbizi wa Afghanistan.

Wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran

 

Iran inatoa misaada hiyo bila ya kujali vikwazo vya kidhulma vya Marekani na vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na maadui dhidi ya wananchi wa Iran. Hata Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amekiri kwa kusema, matatizo yaliyopo katika masuala ya wakimbizi wa Afghanistan yanatokana na vikwazo ambavyo kila kukicha vinaongezeka dhidi ya Iran.

Alaakullihaal, kinachotarajiwa kutoka kwa jamii ya kimataifa ni kutafuta njia za kimsingi za kukabiliana na mgogoro wa ukimbizi kama ambavyo Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yanapaswa kutekeleza vilivyo ahadi zao kwa nchi zinazopokea wakimbizi na kuandaa mazingira salama katika nchi zenye migogoro, ya kuweza kuwafanya wakimbizi hao watamani wenyewe kurejea kwenye nchi zao.  

Maoni