Feb 15, 2020 08:05 UTC
  • Zarif: Kwa ujinga na taarifa ghalati, Marekani imeisukuma Asia Magharibi kwenye ukingo wa shimo la vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia jinai iliyofanywa na Marekani ya kumuua kigaidi, shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kusisitiza kuwa, kwa ujinga wake na kwa kutegemea taarifa ghalati na zisizo sahihi, Marekani imelisukuma eneo la Asia Magharibi kwenye ukingo wa shimo la vita vikubwa.

Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo mapema leo asubuhi katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya NBC ya Marekani pambizoni mwa Mkutano wa Usalama wa Munich, Ujerumani, na kuongeza kuwa, mwezi Januari mwaka huu wakati mgogoro ukiwa umepamba moto baada ya viongozi wa White House kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, alituma barua isiyo nzuri hata kidogo ya kutoa vitisho kwa Iran lakini Tehran ilitoa majibu makali kwa hatua hiyo. 

Aidha Zarif ameishutumu serikali ya Marekani kwa kuanzisha mgogoro dhidi ya Iran na kusema kuwa, kumalizika mgogoro huo kutategemea kurudi nyuma Trump katika siasa zake na kwamba Marekani ndiyo inayobeba dhima ya vitendo vyake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dk Mohammad Javad Zarif (kulia) katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, mjini Munich, Ujerumani, Feb 14, 2020

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amekanusha madai ya uongo ya Marekani ya eti makundi ya muqawama ya Iraq na Lebanon yanadhibitiwa na Tehran akisisitiza kuwa, kabla ya kuuliwa kigaidi; Kamanda Soleimani alikuwa katika jitihada za kupunguza machafuko nchini Iraq.

Jana usiku pia Mohammad Javad Zarif alifanya mazungumzo na waandishi wa habari na kusema kuwa, iwapo nchi za Ulaya zitaheshimu ahadi zao ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA, basi Iran nayo itasimamisha mchakato wa kupunguza ahadi zake ndani ya mapatano hayo.

Pambizoni mwa kikao hicho cha Munich, Ujerumani, Dk Zarif ameonana na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Croatia, Oman, China, Finland, Jamhuri ya Zcech, Vatican, Canada, wajumbe wa taasisi ya The Elders na Waziri Mkuu wa Canada.

Maoni