Feb 18, 2020 13:28 UTC
  • Ayatullah Ali Khamenei
    Ayatullah Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa kushiriki kwenye uchaguzi ni wajibu wa kidini, kitaifa na kimapinduzi na haki ya kiraia ya wananchi wote.

Ameashiria nguzo mbili muhimu za "mahudhurio makubwa ya wananchi" na 'kuchagua mtu anayefaa" na kusema: Kushiriki kwenye uchaguzi ni jihadi ya umma, neema na mtihani wa Mwenyezi Mungu ambao pale unapoandamana na mahudhurio ya idadi kubwa ya wananchi hulinda heshima ya Mfumo wa Kiislamu, kuimarisha nchi na kuipa kinga mbele ya njama (za maadui) na kutayarisha mazingira ya kujenga Iran yenye nguvu kubwa zaidi.  

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya maelfu ya wananchi wa Azarbaijan Mashariki huko kakazini mwa Iran waliokwenda kuonana naye. Amesisitiza kuwa, macho ya marafiki na maadui yameelekezwa kwenye uchaguzi wa tarehe 21 Februari hapa nchini na kuongeza kuwa: Njia pekee ya kuwavunja moyo maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuwa na Iran imara na yenye nguvu, na moja ya vielelezo vya Iran imara ni Bunge imara linaloweza kupasisha sheria zinazohitajika na kuilinda nchi kwa kuiongoza serikali katika njia inayofaa. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria baadhi ya ripoti zinazosema kuwa, mojawapo ya nchi kaidi za Ghuba ya Uajemi zimetoa kiwango kikubwa cha dola, fedha za mafuta, kwa chombo kimoja cha habari cha Uingereza kinachotangaza kwa lugha ya Kifarsi kwa ajili ya kuwashwishi Wairani ili wasiwachague wagombea wenye mielekeo na itikadi za kimapinduzi na kuongeza kuwa: Ripoti hiyo inaonesha ni kwa kiwango gani ubora na jinsi ya kuchagua vilivyo na umuhimu mkubwa. 

Image Caption

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amezungumzia bwabwaja za hivi karibuni za maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu Iran na uchaguzi na kusema: Marekani ilitaka kulidhibiti eneo la magharibi kwa Asia kupitia mauaji yake ya kigaidi dhidi ya Kamanda Qassem Soleimani ambayo yalikuwa na taathira kubwa katika eneo hilo, lakini mambo yalikwenda kinyume na lengo hilo; na maandamano makubwa yaliyofanyika dhidi ya Marekani mjini Baghdad, masuala ya Syria na Aleppo na kadhia nyingine za kanda hii vimekwenda kinyume kabisa na matakwa ya Wamarekani. 

Ayatullah Ali Khamenei amesema adui hakupata pigo katika tukio la mauaji ya kigaidi ya Shahidi Soleimani pekee bali daima amekuwa akipata vipigo na kushindwa mbele ya taifa la Iran katika vita vya kipindi cha miaka 40 iliyopita. Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita Wamarekani wametumia silaha zote za kisiasa, kijeshi, kiusalama, kiuchumi, kiutamaduni, vyombo vya habari na kila wenzo uliopatikana kwa ajili ya kuangusha utawala wa Kiislamu hapa nchini lakini Mfumo wa Kiislamu haujaondolewa madarakani, na kinyume chake, umeimarika zaidi mara elfu moja na Marekani imedhoofika kuliko hapo kabla.

Umaskini umeongezeka nchini Marekani

Akieleza jinsi Marekani inavyozidi kudhoofika siku baada ya nyingine, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchi hiyo imejiremba na kuitia vipodozi sura yake ya kidhahiri na kuongea kuwa: Marekani ambayo hii leo inadaiwa dola bilioni elfu 22 inahesabiwa kuwa nchi yenye deni kubwa zaidi duniani, na tofauti za kimatabaka nchini humo zinatisha na ndizo kubwa zaidi kuliko kipindi kingine chochote.

Ubaguzi umeshika kasi zaidi huko Marekani baada ya Trump kushika madaraka

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria takwimu za kutisha za ubaguzi, tofauti iliyopo baina ya matabaka, umaskini na uhalifu nchini Marekani vinavyoangamiza uhai nchini humo mithili ya ukoma na kusema: Kama ambavyo haiba na ukubwa wa meli maarufu ya Titanic havikuzuia kughariki kwa meli hiyo, vivyo hivyo, juhudi za kurembesha sura ya dhahiri ya Marekani na haiba yake havitazuia kughariki nchi hiyo."   

Maoni