Feb 19, 2020 08:02 UTC
  • Uchaguzi na uwezo unaozidi kuongezeka wa taifa la Iran mkabala wa Marekani kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumanne asubuhi alikutana na maelfu ya wananchi kutoka mkoa wa Azerbaijan Mashariki na kusema kushiriki kwenye uchaguzi ni wajibu wa kidini, kitaifa na kimapinduzi na haki ya kiraia ya wananchi wote.

Kiongozi Muadhamu aliashiria kuhusu nguzo mbili muhimu za "mahudhurio makubwa ya wananchi" na 'kuchagua mtu anayefaa" na kusema: Kushiriki kwenye uchaguzi ni jihadi ya umma, neema na mtihani wa Mwenyezi Mungu ambao pale unapoandamana na mahudhurio ya idadi kubwa ya wananchi hulinda heshima ya Mfumo wa Kiislamu, kuimarisha nchi na kuipa kinga mbele ya njama (za maadui) na kutayarisha mazingira ya kuijenga Iran yenye nguvu kubwa zaidi."

Hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu ambayo imetolewa wakati wa kukaribia uchaguzi wa wa Ijumaa; imesisitiza kuhusu nukta muhimu na za kistratijia ambazo ni kufahamu umuhimu wa kushiriki kwa wingi wananchi katika medani zenye kuainisha hatima. Kushiriki katika upigaji wa kura Ijumaa, 21 Februari kunapaswa kuwa moja kati ya misdaki ya kushiriki katika medani katika muda unaofaa.

Kiongozi Muadhamu alisisitiza kuwa: "Uchaguzi ni jihadi ya umma, ni chanzo cha kupata nguvu nchi na kulindwa heshima ya mfumo wa Kiislamu. Kushiriki kwa wingi wananchi katika upigaji kura, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, kutakuwa chanzo cha baraka na taathhira yenye kuleta mabadiliko katika nchi."

Mara kadhaa sasa wananchi wa Iran wamejitokeza katika medani kwa njia isiyo na kifani katika siku nyeti sana kama vile wakati wa uchaguzi, maandamano ya 22 Bahman na Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo huibua hamasa katika medani hizo na hivyo kuvunja njama za maadui sambamba na kukabiliana na wanaoeneza fitina. Kwa msingi huo wananchi wa Iran wameweza kuthibitisha faida ya kujitokeza kwa wakati katika medani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya sababu ambazo zimepelekea wakuu wa Marekani wajihisi dhaifu mbele ya taifa la Iran ni yale yaliyojiri baada ya hatua yao ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani: Akifafanua, Kiongozi Muadhamu alisema: "Katika kadhia hii, rais wa Marekani na wapambe wake wamefahamu kuwa kitendo chao hakikuwa sahihi kwani wamekosolewa ndani na nje ya Marekani."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akihutubia wananchi kutoka mkoa wa Azerbaijan Mashariki 

Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: " Marekani ilitaka kulidhibiti eneo la magharibi mwa Asia kupitia mauaji yake ya kigaidi dhidi ya Kamanda azizi Qassem Soleimani ambayo yalikuwa na taathira kubwa katika eneo hili, lakini mambo yalikwenda kinyume na lengo hilo; na maandamano makubwa yaliyofanyika dhidi ya Marekani mjini Baghdad, masuala ya Syria na Aleppo na kadhia nyingine za kanda hii vimekwenda kinyume kabisa na matakwa ya Wamarekani. Kwa hivyo bwabwaja za hivi karibuni za maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu Iran zinalenga kufidia kufeli huko. "

Kwa hakika kila wakati wananchi wanapojitokeza kwa wingi, na kujitokeza huko kunazidi kuongezeka, inabainika wazi kuhusu kutokuwa na taathira vitisho na mashinikizo ya adui dhidi ya taifa la Iran.

Kuhusiana na nukta hiyo, kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuhusu namna ambayo moja ya nchi za eneo ilivyotumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kufadhili vyombo vya habari hasimu vya lugha ya Kifarsi vilivyoko Uingereza kwa lengo la kuwaelekeza wananchi wa Iran wasiwapigie kura wanasiasa imara wenye kushikamana kikamilifu na misingi ya mapinduzi katika uchaguzi na kusema: "Nukta hiyo inaashiria umuhimu wa kiwango na namna ya kuchagua."
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, si tu kuwa adui atashindhwa katika kadhia hiyo, bali pia katika kipindi cha miaka 40 iliyopita daima amekuwa akipata pigo na kushindwa na taifa la Iran. Ameongeza kuwa: "Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita Wamarekani wametumia silaha zote za kisiasa, kijeshi, kiusalama, kiuchumi, kiutamaduni, vyombo vya habari na kila wenzo uliopatikana kwa ajili ya kuangusha utawala wa Kiislamu hapa nchini lakini Mfumo wa Kiislamu haujaondolewa madarakani, na kinyume chake, umeimarika zaidi mara elfu moja na Marekani imedhoofika kuliko hapo kabla."

Akieleza jinsi Marekani inavyozidi kudhoofika siku baada ya nyingine, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchi hiyo imejiremba na kuitia vipodozi sura yake ya kidhahiri na kuongeza kuwa: Marekani ambayo hii leo inadaiwa dola bilioni elfu 22 inahesabiwa kuwa nchi yenye deni kubwa zaidi duniani, na tofauti za kimatabaka nchini humo zinatisha na ndizo kubwa zaidi kuliko kipindi kingine chochote.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mfano wa matatizo ya kina nchini Marekani ambayo yameashiriwa na mmoja kati ya maseneta wa nchi hiyo na kusema: "Mwanasiasa huyu wa Marekani anasema serikali ya Trump imeongeza utajiri  wa watu watano ambao ni kati ya matajiri wakubwa zaidi wa Marekani kwa dola bilioni moja na utajiri wa watatu miongoni mwao ni sawa na utajiri wa nusu ya watu wote wa Marekani. Asilimia 80 ya wafanyakazi wa Marekani ni masikini na mshahara wanaopata hautoshi kukidhi maisha yao. Katika kila Wamarekani watano ni mmoja tu aliye na uwezo wa kununua dawa anazotakiwa na daktari kununua na ufa wa utajiri wa Wamarekani wazungu na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika umeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita."

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria takwimu za kutisha za ubaguzi, tofauti iliyopo baina ya matabaka, umaskini na uhalifu nchini Marekani vinavyoangamiza uhai nchini humo mithili ya ukoma na kusema: "Kama ambavyo haiba na ukubwa wa meli maarufu ya Titanic havikuzuia kughariki kwa meli hiyo, vivyo hivyo, juhudi za kurembesha sura ya dhahiri ya Marekani na haiba yake havitazuia kughariki nchi hiyo."   

Tags

Maoni