Feb 19, 2020 12:58 UTC
  • Agnès Callamard
    Agnès Callamard

Tarehe 3 mwezi uliopita wa Januari Rais Donald Trump wa Marekani alikiuka sheria za kimataifa na kutoa amri ya kuuliwa kigaidi aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wenzake kadhaa karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq alikokuwa ameenda safarini kwa mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard ametoa ripoti Kuhusiana na mauaji hayo ya kigaidi akisisitiza kuwa, yalikuwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Callamard amesema mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Kamanda Soleimani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na hatua hiyo ya Marekani inaweza kuweka msingi wa mwenendo mbaya ambao hatimaye utakuwa na maafa makubwa. 

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Mauaji ya kigaidi ya Jenerali Qassem Soleimani yamekanyaga kikamilifu vigezo vinavyohusiana na matumizi ya nchi ya nguvu za kijeshi nje ya mipaka yake. Katika tukio hilo afisa wa serikali alishambuliwa ilhali hapo awali watu wasio maafisa wa serikali walikuwa wakishambuliwa; na hatua hii ni ukiukaji mkubwa wa kanuni na sheria za kimataifa."

Agnès Callamard

Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Kaimu Mkuu wa kikosi cha wapiganaji wa kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hashul Shaabi, Abu Mahdi Al Muhandes wakiwa pamoja na wenzao 8, walishambuliwa na ndege za kivita za askari magaidi wa Marekani alfajiri ya tarehe 3 Januari karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad na kuuliwa shahidi. Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza kuwa, amri ya mauaji hayo ilitolewa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo. Kisingizio kilichotumiwa na Trump kuhalalisha mauaji hayo ni madai kwamba, Kamanda Qassem Soleimani alikuwa safari nchini Iraq kwa shabaha ya kupanga mashambulizi dhidi ya Wamarekani na kambi zao za kijeshi na kwamba shambulizi hilo lilikuwa hatua ya kujihami. Maafisa wa serikali ya Iraq wamepinga vikali madai hayo. Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq, Adil Abdul Mahdi tarehe 5 mwezi huo huo wa Januari alihutubia Bunge la nchi hiyo na kusema kuwa: Kamanda Qassem Soleimani alikuwa safari nchini kwa ajili ya kukabidhi majibu ya serikali ya Iran kwa barua ya Saudi Arabia iliyokuwa imewasilishwa na Baghdad kwa serikali ya Tehran. Matamshi haya ya Waziri Mkuu wa Iraq yaliweka wazi zaidi uongo wa serikali ya Washington kuhusiana na sababu za mauaji hayo.

Adil Abdul Mahdi akihutubia Bunge la Iraq

Ukweli ni kwamba, serikali ya Donald Trump ilikuwa na mpango wa kumuua kigaidi Jenerali Soleimani tangu mwaka mmoja na nuru kabla yake. Ushahidi na matamshi ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani vinaonesha kuwa, Washington ilichukua uamuzi wa kufanya mauaji hayo ya kigaidi miezi kadhaa kabla na ilikuwa ikisubiri wakati na mahala mwafaka kwa ajili ya kutekeleza uhalifu huo. Televisheni ya NBC ya Marekani tarehe 13 mwezi uliopita wa Januari iliripoti kuwa, mwezi Juni mwaka 2019 yaani miezi saba kabla, Donald Trump alitoa amri ya mauaji ya kigaidi dhidi ya kamanda Soleimani iliyoambatana na masharti. Baada ya Iran kutungua ndege ya kivita isiyo na rubani ya Marekani aina ya RQ-4A Global Hawk iliyoingia katika anga ya Jamhuri ya Kiislamu kinyume cha sheria, Trump aliamuru kwamba, iwapo mashambulizi ya jeshi la Iran au makundi yenye mfungamana na Iran yatapelekea kuuawa askari au raia wa Marekani, Washington inapaswa kumuua Kamanda Qassem Soleimani. Baada ya mauaji ya Jenerali Soleimani Trump alidai kuwa, sababu ya mauaji hayo ni kwamba alikuwa "hatari tarajiwa kwa askari wa Marekani" na kwamba "alikuwa akifanya mipango ya kushambulia balozi nne za Marekani". Hata hivyo rais huyo wa Marekani hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Pamoja na hayo matamshi ya maafisa wa ngazi za juu wa Marekani yanapinga sababu zilizotajwa na Trump kuhalalisha mauaji ya kigaidi ya Kamanda Soleimani. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper Jumapili ya tarehe 12 Februari alikadhibisha madai ya Donald Trump kwamba Jenerali Soleimani alikuwa tishio kwa majeshi ya nchi hiyo na kusema, yeye binafsi hajaona ushahidi wowote unaoweza kuthibitisha kuwa, Iran ilikuwa ikipanga kushambulia balozi nne za Marekani.

Mark Esper

Ukweli ni kwamba, katika mtazamo wa makamanda wa jeshi na maafisa wa usalama wa Donald Trump, kuwa pamoja kwa makamanda Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes mjini Baghdad ambao walikuwa vinara wakuu wa Iran na Iraq waliokuwa na nafasi kubwa katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na wakati huo huo walikuwa kikwazo kikuu katika njia ya kutekeleza malengo haramu ya Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia, ilikuwa fursa ya dhahabu ambayo haikupaswa kuachiwa ipite hivi hivi. Ni kwa kutegemea mtazamo huu ndipo White House ikaamuru mauaji ya kigaidi dhidi ya makamanda hao.

Sasa na baada ya Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnès Callamard kuitaja hatua hiyo kuwa ilikiuka sheria na kanuni za kimataifa, hakuna tena shaka kwamba Donald Trump na serikali yake ni wakiukaji wakuu wa sheria za kimataifa na hawasiti kukanyaga sheria hizo kwa ajili ya kutimiza malengo na siasa zao za mabavu.         

Tags

Maoni