Feb 20, 2020 04:28 UTC
  • Raia wawili wa Iran wafariki dunia mjini Qom kwa maradhi ya virusi vya Corona

Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya nchini Iran, amethibitisha habari ya kufariki dunia watu wawili kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona mjini Qom nchini hapa.

Kiyanush Jahanpur aliyasema hayo jana Jumatano na kubainisha kwamba kufuatia ongezeko la matatizo ya kupumua lililoshuhudiwa katika siku za hivi karibuuni mjini Qom, uchunguzi wa vipimo ulithibitisha kesi mbili za maambukizi ya virusi vya Corona. Ameongeza kwa kusema: "Kwa bahati mbaya watu wawili ambao ni wazee na kutokana na upungufu wa vifaa vya tiba katika wodi maalumu za hospitali za mji huo, walipoteza maisha yao kwa maradhi hayo." Wakati huo huo Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) jioni ya jana alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Udaktari wa Iran, Saeed Namaki ambapo sambamba na kumueleza kuwa amepata taarifa za kuthibitika kesi mbili za ugonjwa unaotokana na virusi vya Corona mjini Qom, alitaka kuchukuliwa hatua za dharura kwa ajili ya kuzui na kuwatibu waathirika wa maradhi hayo.

Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge)

Aidha kwa nyakati tofauti Larijani alizungumza pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo, Mohsen Haji Mirzaei na kumpa maelekezo ya lazima yenye lengo la kuzuia maradhi hayo kufika maeneo ya shule kwa kuwapa maelekezo wazazi na wanafunzi. Mbali na hayo Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Iran amemtaka Bahram Sarmast, Mkuu wa Mkoa wa Qom kuitisha kikao cha dharura na kuchukua maamuzi ya haraka kwa ajili ya kuzuia kuenea virusi vya Corona katika maeneo ya umma, shule na vyuo vikuu vya mji huo. Inafaa kuashiria kuwa virusi hivyo viliibuka mwishoni mwa mwaka jana katika mji wa Wuhan nchini China na hadi sasa vimeenea ndani ya zaidi ya nchi 25 za dunia, ikiwemo Marekani, Uingereza, Australia, Thailand, Korea Kusini, Japan, Canada, Ufaransa, Saudi Arabia na Imarati. Kwa mujibu wa takwimu za mwisho, hadi sasa zaidi ya watu 72 wameambukizwa virusi hivyo nchini China huku watu 2000 wengine wakiwa wamepoteza maisha. Kamisheni ya Afya ya Kitaifa ya China imetangaza kuwa, zaidi ya watu elfu 10 na 600 wamepatiwa matibabu kutokana na maambukizi ya maradhi hayo.

Maoni