Feb 20, 2020 12:29 UTC
  • Jeshi la Iran lapokea ndege 8 za kijeshi zilizofanyiwa ukarabati kamili nchini

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepokea ndege 8 za kijeshi ambazo zimefanyiwa ukarabati kamili yaani overhaul ndani ya nchi.

Sherehe za kukabidhi ndege hizo zimefanyika katika hafla ambayo imehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami na Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran.

Ndege hizo zilizokarabatiwa kikamilifu ni zile za kivita aina ya F-4, F-14, F-27, Sukhoi na Mirage na pia ndege za usafiri wa kijeshi za C-130 na 707.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema nchi zenye teknolojia ya kukarabati ndege hizo zilikataa kuipa Iran hata vipuri vidogo kabisa na pia zilikataa kushirikiana katika ukarabati kutokana na hofu ya vikwazo vya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Lakini pamoja na kuwepo vikwazo hivyo, Iran imechukua hatua muhimu katika uga wa usafiri wa anga na sasa imeweza kutekeleza miradi muhimu na hivyo kuvuruga vikwazo vya adui.

Moja ya ndege za kivita zilizokarabatiwa kikamilifu (overhaul) nchini Iran

Hatami amesema kufanya ukarabati kamili au overhaul ni kazi ngumu na ujuzi wa kazi hiyo umekuwa ukihodhiwa na nchi chache zenye uwezo mkubwa duniani lakini sasa Iran imepata uwezo huo. Amesema baadhi ya ndege zilizokarabatiwa zina silaha maalumu kama vile makombora ya cruise yenye uwezo wa kuenda masafa ya kilomita 1,000.  

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema ukarabati wa ndege hizo za kijeshi ni jambo ambalo litaimarisha uwezo wa kijeshi wa Iran na pia kupunguza gharama kwa asilimia 50. 

Tags

Maoni