Feb 21, 2020 02:41 UTC
  • Uchaguzi, kielelezo cha ushiriki mkubwa wa kisiasa na nguvu ya wananchi wa Iran

Uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 41 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unaotarajiwa kufanyika leo Ijumaa unaakisi umuhimu wa chaguzi katika mfumo wa demokrasia ya kidini nchini Iran.

Kushiriki wananchi katika masuala ya kisiasa na mchango na nafasi yao ya moja kwa moja na kwa uhuru katika kuainisha mustakbali wao wenyewe, kunaonyesha umuhimu wa kutiliwa maanani masuala muhimu ya serikali na tawala za kidemokrasia katika kipindi cha miaka 41 ya Mapinduzi ya Kiislamu. Zoezi hili la leo linahusu uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la 11) na ule wa marudio wa Baraza la Wataalamu Wanaumchagua Kiongozi Mkuu wa Iran.

Raia milioni 57, laki 9, na 18 elfu na 159 wa Iran wamekamilisha masharti ya kupiga kura na zaidi ya wagombea elfu saba na 157 wanachuana katika majimbo 208 ya uchaguzi kwa ajili ya viti 290 vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.  

Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu

Kushiriki kwa wingi wananchi katika zoezi la kupiga kura na kuchagua wawakilishi wao katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) mbali na kudhihirisha mwenendo wa kupokezana madaraka katika mojawapo ya nguzo muhimu za mfumo wa demokrasia ya kidini nchini Iran, lakini pia kunaonesha mchango wa wananchi katika kujiamulia mambo yao wenyewe. 

Bunge imara na lenye nguvu huwa na mchango muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na kazi yake ya kutunga sheria zinazohitajika katika nyanja mbalimbali na vilevile lina nafasi muhimu katika siasa za nje za nchi kwa kuchukua maamuzi sahihi yanayoakisi matakwa ya wananchi waliolichagua.

Majlisi ya Ushauri Kiislamu yaani Bunge la Iran lina nafasi na mchango mkubwa pia katika kuimarisha taasisi nyingine za dola hapa nchini kutokana na majukumu mawili maalumu ya wabunge ambayo ni kutunga sheria na kusimamia utendaji wa taasisi za dola ukiwemo utendaji wa serikali. Haya yote hayawezi kutimia bila ya mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi la uchaguzi na kuwachagua wawakilishi wanaofa. Suala hili limeashiriwa na Rais Hassan Rouhani katika kikao cha baraza la mawaziri akisema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi katika uchaguzi wa leo yataitia hasira na kuighadhabisha Marekani. Rais Rouhani amesisitiza kuwa: Kwa umoja na mshikamano wao, Wairani watawaonesha tena Wamarekani kwamba wana nguvu na uwezo mkubwa. 

Rais Hassan Rouhani

Mahudhurio ya wananchi wa Iran katika medani ya siasa na medani nyinginezo kama hii ya uchaguzi wa Bunge katika kipindi chote cha miaka 41 iliyopita ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini yamekwenda kinyume na propaganda chafu za maadui na kushinda njama zao, na kuonyesha kuwa, mahudhurio ya wananchi katika medani hizo muhimu ndio nguzo kuu ya uwezo na nguvu ya Iran.

Kiwango cha ushiriki wa wananchi wa Iran katika masuala ya kisiasa na katika chaguzi za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ambacho kimekuwa cha zaidi ya asilimia 51 ya watu waliokamilisha masharti ya kupiga kura baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, daima kimekuwa cha juu hata zaidi ya kile cha ushiriki wa wananchi katika chaguzi kama hizo kwenye nchi zinaodai kuwa vinara wa demokrasia.

Wairani wakishiriki zoezi la kupiga kura

Japokuwa wananchi wa Iran katika baadhi ya vipindi hawakuridhishwa na utendaji wa baadhi ya serikali za wakati huo lakini suala muhimu zaidi kwao ni kulinda na kutetea Mfumo wa Kiislamu kupitia njia ya kushiriki kwa wingi katika chaguzi za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu. Suala hili limeakisiwa katika matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif ambaye amesema: Uwezo na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu unatokana na wananchi wenyewe, na uchaguzi ndiyo medani ya kudhihirisha na kuonyesha nguvu hizo za wananchi..        

Tags

Maoni