Feb 21, 2020 02:44 UTC
  • Brigedia Jenerali Heidari: Maadui wanaliogopa taifa la Iran kuliko silaha

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui wanaliogopa taifa hili zaidi ya wanavyohofishwa na silaha za nchi hii.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na shirika la habari la Mehr na kuongeza kuwa, "kinachowatia kiwewe maadui wa Jamhuri ya Kiislamu hata zaidi ya silaha za kijeshi, ni taifa kubwa la Iran na uungaji mkono wake kwa mfumo."

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kuzipatia ufumbuzi changamoto na matatizo ndani ya miongo minne iliyopita ya Mapinduzi ya Kiislamu, kutokana na kuhusishwa na kushirikishwa wananchi wa Iran katika maamuzi ya masuala ya nchi yao.

Brigedia Jenerali Kioumars Heidari amesema hayo kuelekea uchaguzi wa Bunge la Iran unaofanyika leo Ijumaa. Maelfu ya wagombea wanachuana katika uchaguzi wa Bunge lenye viti 290, katika maeneobunge zaidi ya 200 katika mikoa yote 31 ya nchi.

Mabango yenye picha za baadhi ya wagombea wa ubunge nchini Iran

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo na shirika la habari la Mehr, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuhusu uungaji mkono wa Iran kwa mataifa yanayodhulumiwa.

Amesema, "madola ya kiistikbari yana uhakika kuwa siku moja, tutawafikia watu wanaodhulumiwa kote duniani na kuwasaidia kukabiliana na madhalimu wao, kama ambavyo mataifa ya Iraq, Syria na Yemen yamekuwa yakipata uungaji mkono wa kiroho wa taifa la Iran katika mapambano yao dhidi ya maadui." 

 

Tags

Maoni