Feb 21, 2020 09:14 UTC
  • Uchaguzi, sherehe ya kitaifa katika kutimia mwaka wa 41 wa Mapinduzi ya Kiislamu

Duru ya 11 ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) imeanza leo Ijumaa tarehe 21 Februari katika mji mkuu Tehran na maelfu ya miji na vijiji katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uchaguzi ni nembo ya demokrasia ya kidini nchini Iran ambayo ilianzishwa kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo kwa wastani uchaguzi mmoja hufanyika kila mwaka hapa nchini. Ni wazi kuwa suala hili linathibitisha wazi nafasi ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ya wananchi katika kuamua na kuainisha mustakbali wa nchi yao pamoja na mustakbali wao wenyewe.

Ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika uchaguzi una ujumbe muhimu wa kitaifa, kieneo na kimataifa. Ujumbe wa kitaifa ni kuwa ushiriki huo ni alama ya kushiriki wananchi kisiasa katika harakati ya kutetea maslahi ya kitaifa. Kuhusu suala hilo, mara tu baada ya kushiriki zoezi hilo muhimu la upigaji kura leo asubuhi, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa siku ya upigaji kura ni siku ya sherehe ya kitaifa na kuongeza kuwa siku ya kupiga kura ni siku ya kuthibiti haki ya kiraia na kitaifa ambapo kwa kupiga kura, wananchi huwa wanataka kushiriki katika uendeshaji wa nchi yao, jambo ambalo ni haki yao ya msingi. Mbali na hayo kupiga kura ni wajibu wa kidini.

Kiongozia Muadhamu vilevile amesisitiza kwamba uchaguzi hudhamini maslahi ya kitaifa na kusema: Hivyo kila mtu anayejali maslahi ya kitaifa atashiriki katika uchaguzi.

Kiongozi Muadhamu akipiga kura katika uchaguzi wa leo Ijumaa

Katika hali ambayo Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuchochea na kuwafanya wananchi wa Iran wasishiriki katika uchaguzi, ni wazi kuwa kushiriki kwao katika duru hii ya 11 ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, kuna ujumbe wa kieneo na kimataifa kwamba watu wa Iran wanaunga mkono Mapinduzi yao ya Kiislamu hata katika mazingira magumu zaidi ya 'vikwazo vya juu zaidi' vya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ushiriki wa kisiasa wa wananchi wa Iran katika chaguzi zote zilizopita na wa mara hii wa duru ya 11  ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni jambo linalothibitisha wazi uwajibikaji wao na kwamba wanafahamu vyema haki yao ya kiraia hata katika mazingira magumu zaidi ya mashinikizo ya maadui.

Ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika chaguzi zote ambazo zimefanyika nchini katika kipindi cha miaka 41 ya umri wa Mapinduzi ya Kiislamu, umeimarisha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika upeo wa kieneo na kimataifa. Ni wazi kuwa nguzo muhimu ya nguvu na usalama wa Iran ni wananchi wenyewe ambao huwa hawashindwi na maadui hata katika mazingira ya hivi sasa ya uadui na ugaidi wa kila aina ukiwemo wa kiuchumi, unaotekelezwa dhidi yao na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Rais Hassan Rouhani akishiriki uchaguzi wa Bunge leo Ijumaa

Safu na foleni ndefu za wapigaji kura ambazo zimeonekana mapema leo asubuhi wakati wa kufunguliwa vituo vya upigaji kura wa duru ya 11 ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Iran (Bunge) kwa mara nyingine tena zimevuruga mahesabu ya watawala wa Marekani na kutoa ujumbe huu muhimu kwa walimwengu kwamba, licha ya kuwepo matatizo kadhaa yanayowakabili, lakini Wairani wangali wako macho na kuwa tayari kutetea maslahi yao kwa nguvu zao zote.

Katika uwanja huo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo ameashiria kwamba kuiamini Iran, ni Wairan kuamini mustakbali wao wa pamoja na kusema kuwa: Siku ya uchaguzi ni kuakisiwa ujumbe huu kwamba Wairani ni Waaminifu (kwa Mfumo wao).

Uaminifu wa Wairani kwa mfumo wao katika miaka 41 iliyopita, unathibitisha wazi kwamba taasisi zao zote za kiserikali zinaungwa mkono na wananchi na leo pia kwa mara ya 38 wananchi wa Iran wamejitokeza kwa kishindo ili kushiriki katika 'sherehe' hii muhimu ya 'kitaifa' na kutetea 'maslahi ya kitaifa' kwa nguvu zao zote.

Tags

Maoni