Feb 21, 2020 14:51 UTC
  • Idadi ya waliofariki kwa COVID 19 Iran yafikia watu wanne, walioathirika ni 14

Idadi ya watu wote waliokumbwa na kirusi cha COVID 19 nchini Iran imefikia 18 ambapo wanne miongoni mwao wamefariki dunia.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Kianoush Jahanpour, mkuu wa kitengo cha habari cha Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran akitangaza kuwa: Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo vipya vilivyochukuliwa, hadi kufikia leo Ijumaa kesi 14 mpya zimethibitishwa za watu waliokumbwa na kirusi cha COVID 19 (aina mpya ya corona).

Jahanpour ameongeza kuwa, aidha watu wengine wawili walioathiriwa na kirusi hicho wamefariki dunia.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Iran, watu watano walithibitika kuambukizwa kirusi hicho kipya cha corona hapo jana, ambapo wawili kati yao waliaga dunia kutokana na uzee na udhaifu wa kinga ya mwili.

Kirusi cha corona ambacho kilizuka na kuenea katika mji wa Wuhan nchini China, hivi sasa kimesambaa katika zaidi ya nchi 25 nyingine duniani ikiwemo Marekani, Uingereza, Australia, Thailand, Korea Kusini, Japan, Canada, Ufaransa, Saudi Arabia na Imarati.

Kwa mujibu wa takwimu mpya, hadi sasa zaidi ya watu 76,000 wameshakumbwa na kirusi cha COVID 19 nchini China na watu wasiopungua 2,200 wameaga dunia kutokana na ugonjwa unaosababishwa na kirusi hicho.

Sambamba na hayo, Kamisheni ya Taifa ya Afya ya China imetangaza kuwa hadi sasa watu zaidi ya 18,000 pia waliokuwa wamekumbwa na kirusi hicho wametibiwa na kupona.../

Maoni