Feb 21, 2020 15:00 UTC
  • Vyombo vingi vya habari duniani vyaakisi wananchi wa Iran walivyoshiriki kwa hamasa katika uchaguzi

Vyombo mbalimbali vya habari duniani vimeakisi namna wananchi katika Iran ya Kiislamu walivyoshiriki kwa wingi na kwa hamasa katika uchaguzi wa Bunge la 11 na uchaguzi mdogo wa Baraza la 5 la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi uliofanyika leo nchini kote.

Kanali ya televisheni ya France ilionyesha taswira za zoezi la upigaji kura lilipoanza mapema leo katika uchaguzi wa Bunge la 11 la Iran na kuripoti kuwa, upigaji kura unafanyika nchini licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani na kuripotiwa habari za kuenea virusi vya corona katika baadhi ya miji.

Tovuti ya habari ya televisheni ya CNN imeashiria katika ripoti yake kuhusu uchaguzi uliofanyika nchini Iran kwa kuzungumzia mivutano iliyopo baina ya Iran na Marekani na kueleza kwamba: Wataalamu wa mambo wanaitakidi kuwa, mpira sasa uko uko kwenye uwanja wa Marekani, na si hasha Washington ikalazimika kuangalia upya sera zake kuhusu Iran.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa, uchaguzi wa bunge umefanyika sambamba na mashinikizo yanayozidi kuongezeka ya Washington dhidi ya Tehran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia lakini yumkini ukazidi kuuimarisha utawala nchini Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, Ayatullah Khamenei akipiga kura katika uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu, Februari 21

Televisheni ya Aljazeera ya Qatar iliripoti kuwa ushiriki wa wananchi kuanzia saa za awali za upigaji kura ulikuwa mkubwa; na sambamba na kusitisha matangazo yake ya kawaida iliakisi mubashara tukio la kupiga kura Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei katika Husainiya ya Imam Khomeini mapema leo.

Mbali na Redio ya kimataifa ya Ufaransa (RFI) na Kanali ya televisheni ya Al-Arabiyyah zilizoakisi pia uchaguzi wa leo hapa nchini, televisheni za Al-Masirah, Al- Mayadeen, Al-Manar na Falastin-Alyaum, zilionyesha moja kwa moja taswira za zoezi la upigaji kura nchini kote na kuripoti kuwa wananchi walijitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo wa Bunge na Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa kumchagua Kiongozi Mkuu kuanzia saa za awali za upigaji kura.../

Tags

Maoni