Feb 25, 2020 15:48 UTC
  • Iraj Harirchi
    Iraj Harirchi

Naibu Waziri wa Afya wa Iran amethibitisha kuwa amepatwa na virusi vya Corona lakini amesisitiza kuwa, nchi hii itashinda janga la virusi hivyo wiki chache zijazo.

Iraj Harirchi amesema, kwa sasa amewekwa katika karantini ambako anapewa matibabu na kwamba hali yake ya kiafya ni nzuri kwa ujumla japokuwa anasumbuliwa na homa na uchovu.

Harirchi amesema ana uhakika kwamba, Iran itashinda mlipuko wa virusi vya Corona katika wiki kadhaa zijazo akisisitiza kuwa, nchi hii ina zana na matibabu madhubuti.

Kesi za virusi vya Corona nchini Iran zilianza kurekodiwa katika mji wa Qum ulioko katikati mwa nchi na hadi sasa vimesababisha vifo vya watu 15. Watu wengine 95 wameambukizwa virusi hivyo.

Itakumbukwa kuwa, wataalamu wa Iran wamefanikiwa kutengeneza kifaa maalumu cha kupima kirusi cha Corona. Kifaa hicho ni cha kwanza cha aina hiyo kuundwa hapa nchini. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, kifaa hicho cha kupima kirusi cha Corona kimeundwa na wataalamu wa Iran katika Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Homa ya virusi vya Corona iliripotiwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan mkoani Hubei mashariki mwa China na sasa mbali na kuathiri mikoa 30 ya nchi hiyo homa hiyo imeenea katika zaidi ya nchi 30 zikiwemo Iran, Marekani, Uingereza, Australia, Italia, Thailand, Korea Kusini, Japan, Canada, Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati.

Tags

Maoni