Feb 26, 2020 12:43 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani ifikirie maelfu ya watu waliofariki nchini humo kwa homa ya mafua

Kufuatia matamshi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran yaliyotolewa na viongozi wa Marekani, Rais Hassan Rouhani amesema: Marekani inapasa ishughulishwe na kufikiria maelfu ya watu waliofariki nchini humo kutokana na homa ya mafua.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kudai kwamba, Marekani ina wasiwasi mkubwa kuwa huenda Iran imeficha taarifa zaidi kuhusiana na maambukizi ya kirusi cha corona.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Mawaziri mapema leo, Rais Rouhani amesisitiza kuwa, kirusi cha corona kisigeuzwe kuwa silaha ya maadui ili kusimamisha shughuli za kazi na uzalishaji nchini na akaongeza kwamba: Takwimu zinaonyesha kuwa, katika miaka ya karibuni ndani ya Marekani watu kati ya elfu 12 hadi laki moja wamepoteza maisha kutokana na maambukizi ya kirusi cha homa ya mafua.

Dakta Rouhani amebainisha kuwa: Katika miaka miwili ya karibuni, na kwa kutumia vikwazo na propaganda, Marekani na maadui wengine wa Iran wamejaribu kila mara kusimamisha uzalishaji na shughuli za kiuchumi ndani ya Iran, lakini njama zao hizo zimezimwa kutokana na kuwa macho wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran imechukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na kirusi cha corona na akaongeza kwamba: Kirusi cha corona, nacho pia kitatoweka kwa uratibu na ushirikiano wa wananchi na serikali ya Iran.

Maambukizi ya kirusi cha corona yalianzia katika mji wa Wuhan nchini China Desemba mwaka uliopita wa 2019 na inavyoonesha chanzo chake ni wanyama wasio wa kufuga.

Mbali na mikoa 30 ya China, hivi sasa kirusi hicho kimesambaa kwenye nchi zaidi ya 36 duniani zikiwemo za eneo la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, hadi sasa watu zaidi ya 81,000 wameambukizwa kirusi hicho katika nchi mbalimbali duniani, ambapo zaidi ya elfu thelathini kati yao wamepata nafuu na wengine zaidi ya 2,700 wameaga dunia.../

 

Tags

Maoni