Feb 27, 2020 13:07 UTC
  • Hemmati: Iran ina uhusiano wa kimataifa wa kibenki usioweza kuwekewa vikwazo

Gavana wa Benki Kuu ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imebuni uhusiano wa kibenki wa kimataifa usioweza kuwekewa vikwazo na wala usiohusiana na jopokazi la eti kupambana na utakatishaji wa fedha chafu linalojulikana kwa kimombo kama Financial Action Task Force (FATF).

Abdolnaser Hemmati amesema katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "nchi yetu imefanikiwa kuunda uhusiano wa kibenki na mfumo wa mabadilisho ya kifedha wa kimataifa usioweza kuwekewa vikwazo na ambao upo nje ya fremu ya FATF."

Amesisitiza kuwa, Benki Kuu ya Iran kwa kushirikiana na sekta nyingine za uchumi itaendeleza jitihada zake za kuhakikisha kuwa mahitaji endelevu ya kibiashara ya Iran yanakidhiwa.

Gavana wa Benki Kuu ya Iran ameeleza bayana kuwa, mfumo wa kifedha wa Iran uko imara na kwamba mtikisiko wa kupanda kwa bei ya fedha za kigeni unaoshuhudiwa hivi sasa nchini utashughulikiwa ndani ya siku chache zijazo.

Taasisi hiyo ya FAFT ina makao makuu yake mjini Paris

Itakumbukwa kuwa, kundi la FATF ambalo linadai kupambana na utakatishaji wa fedha chafu mnamo Februari 21 lililiweka jina la Iran katika orodha yake nyeusi, hatua ambayo imekosolewa vikali na maafisa wa serikali ya Tehran.

Iran inasisitiza kuwa, kitendo hicho ni cha kisiasa chenye lengo la kuendelea kuliweka chini ya mashinikizo taifa la Iran.

Tags

Maoni