Mar 03, 2020 07:35 UTC
  • Zarif akosoa ukatili na ghasia zilizopangwa dhidi ya Waislamu India

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali ukatili na ghasia zilizoratibiwa dhidi ya Waislamu nchini India, akisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro uliopo ni kufuata sheria na mazungumzo ya amani.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana usiku, ambapo ameitaka serikali ya New Delhi kukomesha ukandamizaji huo dhidi ya Waislamu.

Katika ujumbe huo, Dakta Zarif amesema, "kwa karne nyingi, Iran imekuwa rafiki wa India. Tunaziomba mamlaka husika nchini India kuhakikisha kuwa jamii yote ya India wanakuwa katika hali nzuri, na sio kuruhusu ukatili usio wa kibinadamu kutawala."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, "njia ya kusogea mbele ni majadiliano ya amani na utawala wa sheria." 

Hivi karibuni Bunge la India linalodhibitiwa na Wahindu wenye misimamo mikali lilipasisha sheria ya kibaguzi ambayo imesababisha machafuko makubwa na hadi sasa watu 43 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika ghasia zilizosababishwa na sheria hiyo iliyo dhidi ya Waislamu nchini humo.

Ukatili dhidi ya Waislamu mjini New Delhi, India

Hapo jana pia, Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akizungumza na waandishi wa habari alieleza masikitiko yake kuhusiana na ukandamizaji wanaofanyiwa Waislamu nchini India na kusema kuwa, Tehran inaitambua India kuwa ni nchi ya uvumilivu wa kidini; hivyo habari za kuwepo ukandamizaji dhidi ya Waislamu nchini humo ni suala linalotia wasiwasi mkubwa.

Maandamano ya kulaani ukandamizaji huo dhidi ya Waislamu wa India yamefanyika katika nchi zaidi ya 18 duniani ikiwemo Marekani na hata nchi za Ulaya.

 

 

Tags

Maoni