Mar 21, 2020 08:07 UTC
  • China yaendelea kuipatia Iran misaada ya vifaa vya tiba kwa ajili ya kukabiliana na corona

Shehena nyingine nne za vifaa vya tiba za msaada wa serikali na wananchi wa China kwa ajili ya kukabiliana na kirusi cha corona zimetumwa hapa nchini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, zaidi ya tani 30 za vifaa vya tiba na afya zimetumwa mjini Tehran katika muendelezo wa misaada ya kibinadamu inayotolewa na serikali na wananchi wa China kwa Iran kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya kirusi cha corona.

Hadi sasa zaidi ya shehena 18 za vifaa vya matibabu pamoja na misaada ya vifaa vya kiafya na dawa kutoka kwa wananchi na serikali ya China zimetumwa nchini Iran kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Licha ya kuenea maambukizo ya kirusi angamizi cha corona duniani ikiwemo nchini Iran pamoja na ulazima wa kupambana nacho mtawalia na kwa kila hali, Marekani ingali inashikilia mtazamo wake wa kuendeleza vikwazo dhidi ya Iran kupitia sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa huku ikiendelea kila mara kutangaza vikwazo vingine vipya dhidi ya Tehran.

Itakumbukwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo haramu na vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran. Waziri Zarif alieleza katika barua hiyo: "Pamoja na uwezo wa kitaalamu ulionao mfumo wa afya wa Iran, lakini vikwazo na masharti inayotoa Marekani ili kukwamisha uuzwaji dawa na zana za tiba, yametatiza vibaya jitihada za kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona nchini Iran".../

Tags

Maoni