Mar 25, 2020 07:18 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran:  Marekani itaondoka Yemen kwa kushindwa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali hujuma ya kijeshi ya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen na kusisitiza kuwa: "Marekani kwa mara nyingine itaondoka Yemen kwa kushindwa."

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa Jumanne kwa munasaba wa kuingia mwaka wa sita tokea Yemen ivamiwe kijeshi na muungano wa Saudia imeongeza kuwa: "Hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen inaendelea katika hali ambayo, Marekani na nchi zingine si tu kuwa zimefumbia macho jinai za kivita zinazotekelezwa na muungano vamizi bali pia zinaendelea kuuzia mungano huo silaha na kuupa himaya ya kijasusi na kilojistiki." Taarifa hiyo imesema, kwa kuzingatia nukta hiyo, Marekani na washirika wake wanapaswa kuwajibishwa kwa sababu ni wahusika wa jinai dhidi ya Wayemen.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema hivi sasa Marekani inaendelea kuongeza wanajeshi wake katika maeneo mbali mbali ya Yemen na kuongeza kuwa: "Marekani imethibitisha kuwa, katika kila nchi ambayo imejiingiza katika eneo, matokeo yake yamekuwa ni ukosefu wa usalama na uporaji wa utajiri wa nchi hizo."

Taarifa hiyo aidha imesema mashirika ya kimataifa yamethibitisha kuwa asilimia 80 ya watu wa Yemen, yaani takribani watoto na wanawake milioni 25 wa Yemen wanahitajia msaada wa kibinadamu na kuongeza kuwa: "Vikwazo vya kidhalimu na vilivyo dhidi ya ubinadamu pamoja na jinai ambazo wamewatendea watu wa Yemen ni chanzo cha maafa ya kibinadamu nchini humo ambayo yametajwa kuwa maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani katika karne."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitza kuwa, tokea awali, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, mgogoro wa Yemen hauna utatuzi wa kijeshi na imewasilisha mpango wa nukta nne wa utatuzi wa mgogoro huo. Katika mpango huo, Iran imesisitiza kuhusu usitishwaji vita mara moja, kufikishwa misaada ya kibinadamu, kuondolewa mzingiro wa kidhalimu na kuanza mazungumzo ya Wayemen kwa Wayemen baina ya makundi yote na hatimaye kuundwe serikali jumuishi ya kitaifa.

Hujuma ya kinyama ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen ilianza Machi 26 mwaka 2015.

Tags

Maoni