Mar 25, 2020 07:50 UTC
  • Rada ya Jeshi la Iran aina ya Fat'h 14 yazuia ndege vamizi ya F-18

Rada ya Jeshi la Anga la Iran imefanikiwa kuitambua na kuionya ndege ya kisasa ya kivita aina ya F-18 iliyokuwa inakaribia kukiuka anga ya Iran kusini mwa nchi.

Taarifa zinasema rada hiyo aina ya Fat'h 14 iliionya ndege hiyo mara kadhaa na kwa msingi huo ndege hiyo aina ya  F-18 Super Hornet, inayoaminika kuwa ya Jeshi la Marekani, ikalazimika kurejea ilikotoka. Jeshi la Anga la Iran liliionya ndege hiyo kuwa, iwapo ingeendelea na mkondo wake wa kuelekea katika anga ya Iran, ingetunguliwa kwa makombora ya kujihami angani.

Kwa mujibu wa clipu ya video ya majibizano hayo ya rada ambayo imetangazwa na Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB), tukio hilo lilijiri Machi 20 katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia.

Shirika la Habari la Sputnik limesema hatua hiyo ni muhimu kiteknolojia na kisaikolojia na ni ishara ya uwezo wa juu wa Jeshi la Anga la Iran ambalo lina mifumo kadhaa ya vita vya kielektroniki.

Mfumo wa  Rada wa Fat'h 14

Mfumo wa Rada wa Fat'h 14, ambao umeundwa kikamilifu nchini Iran, ulizinduliwa mwaka 2015 na una uwezo wa kioparesheni wa kilomita 600 na unaweza kutambua chombo kinachoruka juu kabisa. Hadi sasa Marekani haijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo ambalo lilijiri siku chache tu baada ya gazeti la New York Times kuripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alikuwa anataka 'hatua kali' zichukuliwe dhidi ya Iran wakati ikijishughulisha na mapambano dhidi ya kirusi cha corona.

Itakumbukwa kuwa tarehe 20 Juni mwaka jana, ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya Marekani aina ya Global Hawk ilitunguliwa na kuteketezwa na kikosi cha anga za mbali cha IRGC baada ya kuvuka mpaka wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu wametangaza kuwa kuangushwa kwa droni hiyo ya kisasa kabisa ya Marekani ni jibu kali na la wazi kwa uchokozi wa aina yoyote itakaojaribu kuufanya Washingtin dhidi ya ardhi ya Iran.

 

Maoni