Mar 25, 2020 13:12 UTC
  • Uwezo wa ndani na matumaini ya kulishinda janga la corona nchini Iran

Sambamba na juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya ya Iran katika kupambana na virusi vya corona, jeshi la taifa pia limeanzisha jitihada kubwa za kudhibiti na hatimaye kukomesha kabisa maambukizi ya virusi hivyo hapa nchini.

Baada ya virusi vya corona kuanza kuenea nchini Iran, asasi zote za sekta ya afya na matibabu, viwanda, taasisi za masuala ya kielimu na kisayansi, jumuiya za kiraia na kadhalika zilijitosa katika medani chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Kupambana na Virusi vya Corona kwa ajili ya kulinda uhai wa wananchi. Utumiaji wa nyenzo zote za kitiba katika nyanja mbili tofauti za kutoa matibabu na kufanya uhakiki ikiwa ni pamoja na mafanikio ya kutengeneza chombo maalumu cha kupima na kugundua virusi vya corona na vilevile mikakati ya kutengeneza chanjo na dawa ya virusi hivyo, ni kielelezo cha azma kubwa ya Wairani ya kuibuka na ushindi mbele ya changamoto hiyo kubwa licha ya vikwazo dhalimu vya Marekani.

Jeshi la Iran likipambana na corona

Kuhusiana na suala hili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumapili iliyopita aliashiria miaka 40 ya tajiriba kubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na changamoto na matatizo ya aina mbalimbali na kusema kuwa: Nchi hii ina uwezo mkubwa na suhula nyingi, na ni wadhifa wa viongozi kutambua uwezo huo na kutumia vipawa vya vijana waumini, wenye ari na wachapakazi. 

Sambamba na jihadi kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu inayofanywa na "walinzi wa afya" (madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kote nchini) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19 (corona) Jeshi la Iran pia limejitosa katika medani hiyo kuhakikisha kwamba, janga hilo linatokomezwa kikamilifu hapa nchini. 

Katika uwanja huo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) limeanzisha kampeni kubwa ya mpango wa taifa wa afya kwa kuanzisha hospitali kadhaa za muda katika miji na vijiji vya Iran. Jeshi la Iran pia limechukua hatua haraka na kuanza kutengeneza vifaa na dawa za kukabiliana na maambukizi ya corona kama barakoa (maski) dawa na mada za kunawia mikono, na vilevile kunyunyizia dawa za kuua virusi hivyo katika meneo hatarishi ya miji na vijiji vya Iran. Jeshi hilo pia limetayarisha vituo maalumu vya mapumziko ya watu waliotibiwa na kupona virusi vya corona katika maeneo mbalimbali ya Iran kikiwemo kile kilichowekwa katika eneo la maonyesho ya kimataifa mjini Tehran chenye vitanda zaidi ya elfu mbili.

Sepah wakiwa kazini

Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Iran, Brigedia Jenerali Muhammad Khakpoor amesema kuwa, maeneo elfu tatu kote nchini Iran na maeneo mia moja mjini Tehran yanashughulikiwa na kunyunyiziwa dawa za kufubaza virusi vya corona.

Hatua zote zilizochukuliwa na zinazochukuliwa kote nchini zinaonyesha kuwa, nguvu na uwezo wa kitiba wa Iran ni miongoni mwa nyenzo muhimu sana kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Utumiaji wa nyenzo zote za kitaifa katika uwanja huo unakumbusha hamasa kubwa na tajiriba ya kihistoria ya Iran katika kipindi ca miaka 40 iliyopita ambapo Wairani wameweza kuvuka misukosuko na mashaka mengi kwa kutegemea uwezo wao wa ndai ya nchi.

Wahudumu wa afya wa Iran

Kwa sasa Iran pia inakabiliana na cangamoto ya kimataifa inayojulikana kwa jina la COVID-19 na hapana shaka kuwa, itafanikiwa kushinda na kuvuka salama changamoto hii kutokana na ushirikiano, umoja na jihadi kubwa inayofanywa na asasi zote za serikali, makundi ya kujitolea ya wananchi na wanajihadi wa sekta ya afya.    

  

Maoni