Mar 26, 2020 04:49 UTC
  • Wataalamu wa Iran wapata njia mpya ya kutibu ugonjwa wa Corona

Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Udaktari mjini Abadan, mkoa wa Khuzestan , kusini magharibi mwa Iran, ameelezea mafanikio ya timu ya utafiti wa maradhi ya kuambukiza katika chuo hicho, katika kuwatibu wagonjwa wa virusi vya Corona na kusimamisha vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo.

Shokraleh Salmanzadeh, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Udaktari mjini Abadan aliyasema hayo Jumatano ya jana na kubainisha kwamba uchunguzi athirifu wa dawa dhidi ya virusi iliyojaribiwa kwa wagonjwa mahututi wa virusi vya Corona na kulazwa katika vyumba vya usimamizi maalumu wa hospitali (ICU) katika hospitali ya Taleghani mjini hapo, umekuwa na mafanikio ya kutibiwa wagonjwa hao na kupunguzwa muda wa kulazwa kwao hospitalini.

Shokraleh Salmanzadeh, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Udaktari mjini Abadan

Sara Mubarak, Naibu Mkuu wa Mafunzo na Utafiti na mkuu wa timu ya uchunguzi wa maradhi ya kuambukiza katika chuo hicho pia amesema kuwa tangu kulipoanza kusambaa virusi vya Corona nchini Iran, mkoa wa Khuzestan na maeneo ya karibu na chuo hicho cha Taaluma ya Udaktari mjini Abadan timu ya watafiti ya chuo hicho ilichukua uamuzi wa kutumia dawa ambayo itasaidia kutibu haraka maradhi hayo. Virusi vya Corona viliibuka mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2019 katika mji wa Wuhan wa mkoa wa Hubei nchini China ambapo mbali na China vimezikumba nchi nyingine za dunia zaidi ya 197. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, hadi sasa zaidi ya watu laki nne na elfu 71 wameambukizwa virusi hivyo kote duniani ambapo zaidi ya laki moja na 14 elfu wamepona na zaidi ya elfu 21 wamefariki dunia.

Tags

Maoni