Apr 05, 2020 02:53 UTC
  • Iran yajitosheleza katika kuzalisha vifaa vya kupambana na corona

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia Daktari Sorena Sattari ametangaza habari ya kujitosheleza Iran katika uzalishaji wa vifaa vya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Daktari Sattari aidha amesema, hivi sasa kuna mashirika mawili ya ndani ya Iran yenye uwezo wa kuzalisha vifaa laki moja kwa wiki vya kutambua wagonjwa wa corona na kwamba kwa vile shirika jingine limejitokeza humu nchini kuomba idhini ya kuzalisha vifaa hivyo, sasa Iran haihitajii tena kuagizia zana hizo kutoka nje ya nchi.

Vile vile amesema, mashirika mengine mawili ya Kiirani hivi sasa yanazalisha vifaa vya Ventilator vya kusaidia wagonjwa kupumua, hivyo hospitali za Iran hazihitajii tena kuagizia vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Mapambano dhidi ya kirusi cha corona nchini Iran

 

Makamu huyo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema, kifaa hicho kinaweza kubadilisha kitanda cha kawaida kuwa kitanda cha ICU na kuongeza kuwa, hadi sasa tatizo la mashirika mengi lilikuwa ni uzalishaji wa kifaa hicho, lakini baada ya mashirika mengine mawili ya Iran kuingia kwenye uzalishaji wa Ventilator, tatizo limeshaondoka, tena kwa gharama ya chini ikilinganishwa na vifaa kama hivyo vilivyokuwa vinaagiziwa kutoka nje.

Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, Daktari Sattari amesema, mashirika mengi ya Iran hivi sasa yanafanya utafiti wa kina katika uwanja wa protokali za madawa ya kuweza kuponya corona na kwamba kuna mamia ya majaribio yanafanyika humu nchini sasa hivi kama sehemu ya jitihada hizo za usiku na mchana za kusaka dawa za kutibu ugonjwa wa COVID-19.

Maoni