Apr 05, 2020 11:48 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani was Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kazi za kiuchumi na za kati zisizo na hatari ya maambukizi ya virusi vya corona zinaweza kuanza tena hapa nchini tarehe 11 mwezi huu wa Aprili sambamba na kuchunga na kuheshumu protokali zote za afya.

Akihutubia kikao cha Tume ya Taifa ya Kupambana na Corona hii leo Jumapili, Rais Hassan Rouhani ameashiria pendekezo lililotolewa na Wizara ya Afya la kuanza kazi na shughuli mbalimbali hapa nchini hatua kwa hatua na kwa mpangilio maalumu na kusema: Shughuli za kiuchumi zinaweza kuanza tena sambamba na kuzingatia protokali zote za afya.

Kuhusu suala la kufunguliwa tena maeneo ya kiibada nchini Iran, Rais Rouhani amesema maeneo matakatifu yataendelea kufungwa hadi tarehe 18 mwezi huu wa Aprili na uamuzi mpya kuhusu maeneo hayo utachukuliwa katika vikao vijavyo.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, taifa zima la Iran limeshikama na kuongeza kuwa, wanaoitakia mabaya Iran wanachukizwa na mshikamano na umoja huo. 

Wakati huo huo Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa, hadi sasa wagonjwa 22,011 wa virusi vya corona wamepona ugonjwa wa COVID-19 na wameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka mahospitalini.

Makumi ya maelfu ya wagonjwa wa corona wamepona nchini Iran

Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran, Daktari Kiaonush Jahanpur amesema kuwa, watu 58,226 wamepatwa na virusi vya corona hapa nchini na kwamba 3,603 miongoni mwao wameaga dunia.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa, hadi sasa zaidi ya watu 1,205,801 wameambukizwa COVID-19 kote duniani, 247,961 miongoni mwao wamepona na wengine zaidi ya 64,973 wamefariki dunia kutokana na maambukizi ya kirusi hicho angamizi.

Tags

Maoni