Apr 06, 2020 12:01 UTC
  • Kukabiliana na corona; kubadilisha tishio kuwa fursa

'Nina matumaini kuhusu mafanikio ya Iran katika kukabiliana na virusi vya corona." Hiyo ni kauli ya Daktari Richard Brennan, mkuu wa ujumbe wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliotembelea Iran mwezi uliopita. Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran aliongeza kuwa: "Tunawapongeza na tunajivunia wafanyakazi wa sekta ya tiba Iran kutokana na uchapakazi wao."

Brennan amesema Iran ina moja ya mifumo yenye nguvu zaidi ya afya katika eneo la Mashariki mwa Bahari ya Mediteranea na kuongeza kuwa: "Kubadilishana taarifa ni jambo lenye umuhimu zaidi kwa dunia na hivyo mafanikio ya Iran katika vita dhidi ya corona yanapaswa kufikishwa katika nchi zingine ili zinufaike nayo."

Hadi sasa, bado haujaweza kutabiriwa wakati wa kumalizika au kuangamizwa ugonjwa wa COVID-19 au corona. Baadhi ya weledi wa mambo wanasema itachukua miezi 9 hadi 12 ili chanjo ya corona iweze kuanza kutumiwa. Kwa msingi huo, hadi wakati huo, kazi muhimu zaidi itakuwa ni kuongeza kasi ya kubaini walioambukizwa na kuwaweka katika karantini ili kukata msururu wa maambukizi.

Katika Wizara ya Afya ya Iran na sekta zingine ambazo ziko mstari wa mbele kukabiliana na corona, kuna watu ambao wanafanya jitihada kwa azma imara na thabiti ili kuangamiza ugonjwa huu hatari.  Kuhusiana na nukta hii, siku ya Jumanne mjini Tehran, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Sharif kilizindua mfumo mpya wa kupima na kutambua uwepo wa ugonjwa wa COVID-19 katika mwili wa mwanadamu.

Dakta Hamid-Reza Rabiee, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Shariff  akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo alisema kupiga picha kifua kwa kutumia CT Scan ni njia bora zaidi ya kubaini iwapo mtu ameambukizwa corona au la. Amesema hivi sasa duniani maeneo mawili pekee yaliyo na mfumo kama huo wa Iran kupima COVID-19 ni Chuo Kikuu cha Stanford Marekani na China. Amesema watafiti vijana wa Iran wamefanikiwa kuunda mfumo huo wa kisasa wa kupima corona.

Mfumo huu unafanya kazi kama daktari anayemtibu mgonjwa akiwa mbali na uwezekano wa kufanya makosa ni mdogo sana na unapima mapafu kwa ustadi mkubwa na nukta hiyo ni muhimu sana katika kutibu wagonjwa wa corona.

Shirika moja la Iran linaunda mashine za kupumua (ventilator) 30 kwa siku

Halikadhalika mashirika ya Iran ambayo msingi wake ni elimu yaani knowledge-based hivi sasa yako mbioni kukidhi mahitaji ya vifaa vya kitiba vinavyohitajika katika matibabu ya corona na hadi sasa kumepatikana mafanikio katika uga huo. Kati ya mafanikio hayo hapa tunaweza kutaja mashine za kusaidia kupumua ambayo Kiingereza inajulikana kama ventilator. Mashine hii ni muhimu sana kwa wagonjwa wa virusi vya corona kwa sababu husaidia upumuaji wakati ugonjwa huu unaposababisha mapafu kushindwa kufanya kazi. Mashine hii inaweza kubadilisha kitanda cha kawaida kuwa kitanda cha  ICU au wagonjwa mahututi. Iran sasa imejitosheleza kwa mashine hizi na haihitajii tena kuziagiza kutoka nje.

Sorena Sattari, Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia anasema hivi sasa kuna mashirika mawili ya ndani ya Iran yenye uwezo wa kuzalisha vifaa laki moja kwa wiki vya kutambua wagonjwa wa corona na  sasa hakuna haja tena kuagizia zana hizo kutoka nje ya nchi.

Mashirika ya Iran pia sasa yanaweza kuzalisha maski  na kukidhi mahitaji ya nchi katika wakati huu wa vita dhidi ya corona. Tokea virusi vya corona viripotiwe nchini  mwezi Februari, uzalishaji maski umeongezeka mara nne na katika siku zijazo uzalishaji huo unatazamiwa kuongezeka kiasi kwamba Iran itaweza kuzisaidia nchi za eneo.

Uzalishaji maski umeongezeka katika maeneo yote ya Iran

Daktari Sattari amesema, mashirika mengi ya Iran hivi sasa yanafanya utafiti wa kina katika uwanja wa protokali za madawa ya kuweza kuponya corona na kwamba kuna mamia ya majaribio yanafanyika humu nchini sasa hivi kama sehemu ya jitihada hizo za usiku na mchana za kusaka dawa za kutibu ugonjwa wa COVID-19.

Mafanikio haya yote ni matokeo ya jitihada, azma pamoja na elimu na ni mfano wa wazi wa Ustawi Mkubwa katika Uzalishaji. Hivi sasa nchi zote duniani zinashughulika na vita dhidi ya corona na maambukizi ya ugonjwa huu sasa ni tatizo la kimataifa. Idadi ya walioambukizwa sasa imepindukia milioni na katika hali kama hii kubadilishana uzoefu nchi za dunia kutabadilisha tishio hili kuwa fursa. Nchi nyingi duniani sasa zinasaidiana katika vita dhidi ya corona lakini kuna nchi moja tu ambayo imejitenga na kukaidi matakwa ya kimataifa; nayo ni Marekani. Kwa vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya Iran hasa katika sekta ya tiba, Marekani imeonyesha ni kiasi gani ilivyo mbali na thamani pamoja na vigezo vya ubinadamu.

 

Tags

Maoni