Apr 06, 2020 13:28 UTC
  • Mousavi: Serikali na taifa la Iran halina imani kabisa na maneno ya viongozi wa Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, taifa na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu haina imani kabisa na maneno ya viongozi wa Marekani na kusisitiza kuwa, Tehran haijawahi hata mara moja kuiomba Marekani iitumie misaada ya tiba na matibabu.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari kwa njia ya video na kusisitiza kuwa, walimwengu wote wanaona jinsi vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vilivyo vya kidhulma na vinavyokanyaga sheria. Ameongeza kuwa, licha ya viongozi wa Marekani kudai kuwa bidhaa za madawa, chakula na vifaa vya matibabu hazimo katika orodha ya vikwazo vyake lakini kivitendo viongozi hao wa Marekani wamefunga njia zote za kuingizwa bidhaa hizo nchini Iran.

Vile vile amesema kuwa kuna baadhi ya nchi zinafanya njama za kutumia vibaya ugonjwa wa corona na kubainisha kuwa, Iran inazitaka nchi zote huru na zilizostaarabika duniani zisitekeleze wala kujali vikwazo vya kidhulma na visivyo na msingi vya Marekani ili zifungue uwanja wa ushirikiano wa pamoja na kupambana na tatizo hilo.

Juhudi za kupambana na corona nchini Iran

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vile vile amesema Tehran iko pamoja na mataifa yote yanayopambana na corona duniani na kusema kuwa zaidi ya nchi 30 na taasisi na mashirika ya kimataifa yameisaidia Iran katika kupambana na corona.

Wakati huo huo Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran, Daktari Kiaonush Jahanpur amesema kuwa taifa la Iran kamwe haliwezi kusahau misaada ya China na mataifa mengine katika kipindi kigumu cha kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Daktari Kianoush amesema hayo leo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, serikali na taifa la Iran linazishukuru serikali na mataifa yote yaliyoisaidia katika vita dhidi ya corona hasa China na kwamba kumbukumbu za kihistoria za Wairan haziwezi kusahau misaada hiyo.

Maoni