Apr 06, 2020 13:34 UTC
  • Zaidi ya watu 24,000 wapata afueni ya corona nchini Iran

Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Matibabu ya Iran imetangaza kuwa, kasi ya mchakato wa kuzidi kupata afya njema na afueni kutokana na corona imeongezeka sana humu nchini kiasi kwamba hadi leo mchana watu 24 elfu na 236 walisharuhusiwa kurudi nyumbani kutoka mahospitalini baada ya kupata nafuu kikamilifu.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran ametangaza habari hiyo leo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, watu 60 elfu na 500 wameshaambukizwa ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa.

Vile vile amesema, idadi ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha masaa 24 yalliyopita humu nchini ni watu 136, hivyo idadi ya waliopoteza maisha nchini Iran kutokana na ugonjwa huo hadi hivi sasa ni watu elfu tatu na 739.

Mapambano dhidi ya corona yanafanyika kwa njia mbalimbali nchini Iran

 

Huku hayo yakiripotiwa, jana Rais Hassan Rouhani was Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, kazi za kiuchumi na za wastani zisizo na hatari ya maambukizi ya corona zinaweza kuanza tena humu nchini kuanzia siku ya Jumamosi ya tarehe 11 mwezi huu wa Aprili sambamba na kuchunga na kuheshumu protokali zote za afya.

Akihutubia kikao cha Tume ya Taifa ya Kupambana na Corona jana Jumapili, Rais Rouhani aliashiria pendekezo lililotolewa na Wizara ya Afya la kuanza kazi na shughuli mbalimbali humu nchini hatua kwa hatua na kwa mpangilio maalumu na kusema: Shughuli za kiuchumi zinaweza kuanza tena sambamba na kuzingatia protokali zote za afya.

Hivi sasa nchi zote duniani zimekumbwa na ugonjwa COVID-19 na hadi kufikia leo mchana, watu milioni moja na laki mbili na 84 elfu na 754 (1,284,754) walikuwa wameshathibitishwa kukumbwa na corona kote ulimwenguni.

Maoni