Apr 07, 2020 03:31 UTC
  • Rais Rouhani: Kuzinduliwa INSTEX ni hatua chanya, lakini haitoshi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza kuzinduliwa mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX) na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni chanya, lakini haitoshi kukidhi maslahi yote ya Iran.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kuongeza kuwa, mfumo huo haupaswi kuishia tu katika kuhakikisha kuwa Iran inapokea madawa na chakula, bali uhakikishe kuwa taifa hili linapata mahitaji yake yote.

Ameeleza bayana kuwa, nchi na serikali mbali mbali duniani haziwezi kuvuka kipindi hiki nyeti cha kupambana na janga la corona, bila usaidizi, ushirikiano na kubadilishana tajriba. Nchi za Ulaya chini ya mashinikizo ya Marekani, zimekuwa zikisuasua kutekeleza mfumo huo wa kifedha, ikiwa ni sehemu ndogo ya kuonyesha kuwa EU ingali imefungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Dakta Rouhani ameashiria ugumu wa kupambana na virusi vya corona hapa nchini kutokana na vikwazo haramu vya Marekani na kubainisha kuwa, "Marekani si tu imekiuka sheria za kimataifa kwa kuliwekea taifa hili vikwazo, lakini pia imekanyaga kanuni za afya za mwaka 2005 za Shirika la Afya Duniani (WHO).

Idadi ya waliopoteza maisha nchini Iran kutokana na ugonjwa huo hadi hivi sasa ni watu elfu tatu na 739

Rais wa Iran amesema anatumai nchi rafiki duniani zitaishinikiza Marekani iiondolee nchi hii vikwazo vya kikatili na vya upande mmoja hususan katika kipindi hiki cha kukabiliana na virusi vya corona.

Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mbali na kumtaarifu Rais Rouhani kuhusu hali ya janga la corona katika nchi za Ulaya amebainisha kuwa, anatumai kuzinduliwa mfumo wa INSTEX kutaongeza mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi za Ulaya.

 

Tags

Maoni