Apr 07, 2020 07:34 UTC
  • Mgogoro wa corona umedhihirisha kuwa US haiwezi hata kujiongoza yenyewe

Msaidizi Maalumu wa Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya kimataifa amesema mgogoro wa ugonjwa wa Covid-19 (corona) umeudhihirishia ulimwengu kuwa, utawala wa kibeberu wa Marekani ambao unajiona kuwa kiongozi na mtawala wa dunia umeshindwa hata kujiongoza wenyewe.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twittter, Hossein Amir-Abdollahian amesema, "MgogoroWaCorona umedhihirisha kuwa utawala wa kiimla wa Marekani si tu hauwezi kuisimamia dunia, lakini pia unaonesha kuwa umeshindwa kujiongoza wenyewe."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa, mgogoro huo umebadilisha kikamilifu mfumo wa nidhamu ya dunia na kusisitiza kwamba, dunia ya baada ya corona itakuwa na muundo tofauti, utakaoelekea zaidi katika imani ya utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Rais Donald Trump amelaumiwa kwa kushindwa kudhibiti corona Marekani

Kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Wamarekani 367,507 wameambukizwa virusi vya corona na kuifanya nchi hiyo iongoze kwa idadi ya maambukizi duniani, huku idadi ya waliofariki dunia kwa virusi hivyo nchini humo ikipindukia 10,900.

Tangu mlipuko wa corona uripotiwe mara ya kwanza Disemba mwaka jana 2019, watu zaidi ya 1,350,000 wameambukizwa virusi hivyo hatari kote duniani, huku walioaga dunia wakiwa ni zaidi ya 75,000. Aidha watu 285,000 waliokuwa wameambukizwa virusi hivyo wamepona. 

 

Tags

Maoni