Apr 07, 2020 11:23 UTC
  • Kuendelea kutolewa miito ya kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Kuibuka virusi vya Corona ulimwenguni kumeyafanya mataifa yote ya dunia si tu kwamba, yatumie uwezo wao wa ndani katika sekta ya afya na tiba, bali mataifa hayo sambamba na kutilia mkazo juu ya ulazima wa kuweko ushirikiano wa dunia nzima kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya kukabiliana na virusi vya Corona yanafanya hima pia ya kuchukuliwa hatua za kukabiliana na maradhi hayo sambamba na kuwatibu waathiwa wa virusi hivyo katika mataifa mengine.

Hii ni katika hali ambayo, hatua ya Marekani ya kuziwekea vikwazo baadhi ya nchi ikiwemo Iran, imeifanya Tehran ishindwe kudhamini sehemu ya mahitaji yake muhimu kwa ajili ya kukabiliana na virusi hivyo.

Katika uwanja huo, baadhi ya viongozi wa dunia wamemtaka Rais Donald Trump wa Marekani aiondolee vikwazo Iran katika mazingira ya sasa ili iweze kudhamini mahitaji yake ya dawa, zana za tiba na chakula kupitia masoko ya kimataifa. Katika hatua ya karibuni kabisa, kundi la wanadiplomasia na mawaziri wa zamani wa baadhi ya nchi wamemuandikia barua Rais Donald Trump wa Marekani wakimtaka aiondolee Iran baadhi ya vikwazo hasa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona na juhudi za taifa hili za kukabiliana na virusi hivi.

Barua hiyo inajumuisha, kundi la watu 24 wakiwemo wanadiplomasia waandamizi na maafisawa zamani wa ulinzi wakiwemo makatibu wakuu wanne wa zamani wa Shirika la Kijeshi la Nato, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Hans Blix, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na baadhi ya maafisa wa zamani wa Marekani akiwemo Maledeine Albright, Waziri wa Mashauri ya Kigeni, William Cohen na Chuck Hagel, Mawaziri wa zamani wa Ulinzi, Paul O’Neill, Waziri wa zamani wa Hazina na William Burns mwanadipomasia mashuhuri.

 

Tangu Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi nchini Marekani alichukua mkondo wa kutekeleza sera ya vikwazo vya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran. Kwa muktadha huo, baada ya kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA Mei 8 mwaka 2018, Trump alihuisha vikwazo vilivyokuwa vimesimamishwa dhidi ya Iran na kutekeleza vikwazo hivyo kwa duru kadhaa dhidi ya sekta mbalimbali za uchumi wa Iran.

Licha ya kuwa, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametekeleza sera mbalimbali kwa ajili ya kupunguza taathira hasi ya vikwazo hivyo katika maisha ya wananchi, lakini sekta ya tiba imeathirika mno na vikwazo vya dawa na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Washington. Hali hiyo imepelekea makumi ya watu kufariki dunia hapa nchini wakiwemo wagonjwa wa maradhi maalumu kama wagonjwa wa Epidermolysis Bullosa  unaojulikana pia kama Butterfly Disease kutokana na kutopata dawa wanazohitajia.

Licha ya kuweko hali hii, lakini viongozi wa Marekani wasiotambua utu wala ubinadamu, wameendelea kusisitiza juu ya azma yao ya kutekeleza mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran kwa ajili ya kufikia malengo yao ambapo kubwa zaidi ni kulifanya taifa hili lisalimu amri mbele ya matakwa ya Washington. Brian Hook, mkuu wa "Kundi la Uchukuaji Hatua Dhidi ya Iran" katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alisisitiza hivi karibuni kwamba: Sera yetu ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran itaendelea.

 

Baada ya kuibuka virusi vya Corona na kuhisika zaidi hali ya ulazima wa kupatikana dawa na suhula za tiba, kumeifanya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi na kudhihirisha wazi uhaba wa dawa. Katika uwanja huo, akthari ya mataifa ya dunia yanatilia mkazo juu ya suala la ushirikiano na kusaidiana mataifa ya dunia kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona. Kuendelea vikwazo vya Marekani kumekuwa ni mzigo na shinikizo kubwa mno kwa sekta ya tiba ya Iran na kuifanya ikabiliwe na kibarua kigumu katika kukabiliana na virusi hivi angamizi. Hali hiyo imewafanya viongozi wa Iran akiwemo Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni atangaze wazi kwamba, vikwazo vya Marekani ni kizingiti kikuu kwa taifa hili katika jitihada zake za kukabiliana na virusi vya Corona na hivyo kutoa takwa rasmi la kuondolewa vikwazo hivyo.

Katika hali ambayo, viongozi wa Washington wanaendelea kukana kwamba,  vikwazo vyao dhidi ya Iran havijumuishi huduma muhimu kama dawa na chakula, lakini ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, mbinyo unaotekelezwa dhidi ya mfumo wa benki wa Iran na vikwazo vya kuuza mafuta ya taifa hili nje ya nchi kumeufunga mikono uwezo wa taifa hili katika kudhamini fedha na kushindwa kununua bidhaa za dharura kutoka nje kama dawa na baadhi ya vifaa muhimu kwa ajili ya kuzalisha dawa hapa nchini.

Mazingira haya yamepelekea kuibuka juhudi za kimataifa zinazofanyika kwa lengo la kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Hivi karibuni, wawakilishi wa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa walimwandikia barua Antonio Guterres Katibu Mkuu wa umoja huo, ambapo sambamba na kuashiria kuwa Corona ni adui wa pamoja wa nchi zote, walitahadharisha kwamba, vikwazo vina taathira hasi kwa udhibiti wa maambukizi ya kirusi hicho.

Aidha walisema katika barua yao hiyo kwamba, zama za kukabiliana na hatua za utumiaji nguvu na za upande mmoja, zisizo za kisheria na zenye kukiuka waziwazi sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa ambazo zinachukuliwa na Marekani dhidi ya nchi kadhaa zimewadia na wakaeleza bayana kwamba, ugaidi wa kiuchumi wa Washington dhidi ya Tehran unakinzana wazi na hati ya Umoja wa Mataifa pamoja na maazimio chungu nzima ya Baraza Kuu la umoja huo.

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesisitiza kwamba, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran vinapaswa kupunguzwa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona ili nchi hii iweze kudhamini mahitaji ya dharura.

Akthari ya viongozi wa dunia wanasema kuwa, virusi vya Corona ndio tishio kubwa zaidi baada ya Vita vya Pili vya Dunia na ili kukabiliana navyo, panahitajika hatua za pamoja za walimwengu. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, viongozi wa Marekani sambamba na kutodiriki ukweli na uhakika huu wa sasa, wangali wanapiga ngoma ya kuendeleza siasa zao za upande mmoja.

Tags

Maoni