Apr 07, 2020 14:58 UTC
  • Waziri wa Afya: Iran imeshafikia hatua ya kuuweza ugonjwa wa corona

Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu imefikia hatua ya kuuweza ugonjwa wa corona na akaongeza kwamba, katika siku zijazo baadhi ya mikoa nchini itakuwa imeshafikia kwenye awamu ya kuudhibiti ugonjwa huo.

Saeed Namaki, ameaysema hayo leo katika kikao cha wazi cha bunge na akaongeza kuwa, hakuna mtu aliyekuwa akiamini kwamba katika hali ngumu ya vikwazo Iran itauweza ugonjwa wa corona.

Namaki ameeleza kwamba, hivi sasa watu milioni 71 nchini ambao wameshapimwa ugonjwa wa COVID-19 na akafafanua kuwa, ikiwa idadi ya walioambukizwa corona nchini Iran inaendelea kuongezeka, sababu yake ni kuwa, kutokana na kutekelezwa mpango wa kuwapima watu, mfumo wa kuwachunguza Wairani walioambukizwa virusi vya COVID-19 unafanya kazi ipasavyo.

Aidha Waziri wa Afya wa Iran amesema, hakuna mgonjwa hata mmoja wa corona ambaye ameshindikana kupatiwa huduma hospitali na akabainisha kuwa, hivi sasa kuna asilimia 30 hadi 50 ya vitanda vitupu katika hospitali za mikoa mbali mbali nchini.

Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Ndani Abdoreza Rahmani Fazli ambaye naye pia alihutubia kikao cha wazi cha leo cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) ametoa ripoti mbele ya bunge kuhusu namna wizara yake na wakuu wa mikoa nchini walivyochukua hatua za kudhibiti maambukizo ya virusi vya corona nchini. Katika ripoti yake, Rahmani Fazli amesema, mwenendo wa maambukizo ya corona nchini Iran unaendelea kupungua na mikoa yenye hali hatari ikiwemo ya Gilan na Mazandaran kaskazini mwa nchi imefikia hatua ya kuridhisha.

Kianoush Jahanpour

Wakati huohuo Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu imetangaza kuwa, hadi hivi sasa watu 27,039 wamepata nafuu kikamilifu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitalini humu nchini.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran ametangaza habari hiyo leo Jumanne mbele ya waandishi wa habari huku akibainisha kuwa, hadi hivi sasa watu 62,589 wameambukizwa kirusi cha corona hapa nchini.

Aidha Kiaonush Jahanpur amesema, kwa masikitiko, watu 133 wamepoteza maisha kutokana na COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita na kuifanya idadi ya watu waliofariki dunia hapa nchini kutokana na ugonjwa huo kufikia 3,872.../

Tags

Maoni