Apr 07, 2020 23:32 UTC
  • Mazungumzo ya simu ya Marais wa Iran na Ufaransa; sisitizo juu ya udharura wa kusitishwa vita vya kiuchumi dhidi ya Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alasiri ya juzi Jumatatu Aprili 6 alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambapo sambamba na kukaribisha kwa mikono miwili ubinifu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutangaza kusitishwa vita katika maeneo mbalimbali ya dunia katika kipindi hiki cha virusi vya Corona amesema kuwa, ana matumaini ubunifu huo utamujuisha pia vita vya kiuchumi dhidi ya Iran.

Rais Rouhani ameashiria vita dhidi ya maradhi ya Covid-19 jinsi vilivyokuwa vigumu nchini Iran ikilinganishwa na mataifa mengine ya dunia kutokana na nchi hii kukabiliwa na vikwazo na kueleza kwamba, serikali ya Marekani sanjari na kuwa vikwazo vyake haramu dhidi ya Iran vimekiuka wazi kanuni za kimataifa, lakini katika mazingira ya sasa pia, hatua za sasa za Washington zimekanyaga pia maazimio ya kimataifa ya afya yaliyopasishwa mwaka 2005 na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Jambo lililotiwa mkazo katika mazungumzo ya simu ya Marais wa Iran na Ufaransa kwa namna fulani linahusiana na hatima ya mataifa yote ya dunia. Udharura wa kushirikiana na kubadilishana tajiriba na uzoefu kwa ajili ya kupambana na maradhi ya Covid-19 sambamba na changamoto iliyosababishwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani katika njia ya Iran ya kupata dawa na suhula za tiba kwa ajili ya kuwatibu waathirika wa virusi vya Corona na wakati huo huo kuzuia ueneaji wa virusi hivyo, ni jambo ambalo linapaswa kutathminiwa na kutolewa uchambuzi katika ngazi ya kimataifa.

 

Mtazamo huu unajumuisha pia masuala mengine kama vile usalama wa kieneo suala ambalo limetiliwa mkazo katika mazungumzo ya simu ya Marais wa Ufaransa na Iran. Rais Rouhani amesema kuwa, harakati ya hivi karibuni ya Marekani huko Iraq ni hatua yenye hatari kubwa na tishio kwa usalama wa nchi hiyo na eneo hili kwa ujumla.

Kwa upande wake Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameashiria katika mazungumzo yake na Rais Rouhani juu ya nafasi muhimu na chanya ya Iran katika matukio ya eneo na akasisitiza juu ya udharura wa kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa katika fremu ya kuimarisha amani, uthabiti na usalama wa eneo.

Rais wa Ufaransa ameashiria pia hamu na shauku ya nchi yake ya kupanua ushirikiano wa pande zote na Iran na kueleza kwamba, hatua iliyopigwa katika kuzinduliwa mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX) ni chanya na akaeleza kwamba, ana matumaini kwa kutumiwa mfumo huo, kutaepelekea kuongezeka ushirikiano wa Iran na Ulaya, na kwa muktadha huo mabadilishano ya kifedha baina ya pande mbili yafanyike kwa njia nyepesi zaidi. 

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran

 

Pamoja na hayo, hatua ya awali iliyopigwa katika uwanja huo, ingali ina tofauti kubwa na kile kilichoahidiwa na madola ya Ulaya katika mfumo huo. Hadi sasa zaidi ya nchi 30 na assi kadhaa za kimataifa zimeisaidia Iran katika vita dhidi ya virusi vya Corona. Hata hivyo bado kuna baadhi ya mataifa yangali yanalitumia vibaya suala la virusi vya Corona.

Hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewaonyesha walimwengu kwamba, ni kwa kiasi taifa hilo liko mbali mno na thamani pamoja na vigezo vya ubinadamu. Kama alivyoandika Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran katika ukurasawake wa mtandao wa kijamii wa Twitter ni kuwa: Ukwamishaji mambo na upinzani wa Marekani dhidi ya kudhaminiwa vifaa vya tiba kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona ni kielelezo cha wazi kabisa cha jinai dhidi ya binadamu.

 

Janga la Corona limevuruga kabisa mahesabu yaliyotokana na mfumo kambi moja ulimwenguni ambapo hata Marekani yenyewe haikuwa ikidhani kwamba, ingekabiliwa na changamoto kama hii. Filihali, mataifa yote ya dunia yanapitia kipindi kigumu mno na katika mazingira haya nyeti, nchi zote za dunia zinapaswa kushirikiana na kusaidiana.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kile ambacho kina umuhimu maradufu katika kipindi hiki ni udharura wa kutazama mambo kwa uhalisia na wakati huo huo, kutumia mbinu na utendaji wa kieneo. Kwa mtazamo huo, mazungumzo ya simu ya Marais wa Iran na Ufaransa yaliyofanyika katika kipindi hiki nyeti, yanaweza kutathminiwa kuwa yana umuhimu mkubwa.

Maoni