Apr 08, 2020 11:58 UTC
  • Kuanza awamu mpya ya ustawi wa pande zote na wa kujivunia wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran

Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran alisema jana Jumanne kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 8 Aprili, Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia nchini Iran kwamba awamu mpya ya ustawi wa pande zote na wa kujivunia imeanza katika taasisi hiyo.

Dk Salehi amegusia kuzinduliwa miradi 122 mipya ya taasisi hiyo kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kusema kuwa, katika kipindi hiki cha mashinikizo ya kidhulma ya uistikbari wa dunia dhidi ya Iran ya Kiislamu, Taasisi ya Nishati ya Nyuklia humu nchini inatambua kuwa ni wajibu wake wa kitaifa na kimaadili kudhamini mahitaji ya watu wa afya nchini. Ameongeza kuwa, kufanikishwa malengo makuu yaliyoainishwa katika mchakato wa uzalishaji wa fueli nyuklia pamoja na maendeleo yaliyopatikana katika ujenzi wa taasisi ya pili na ya tatu ya kituo cha nyuklia cha Bushehr sambamba na kustawishwa teknolojia za kisasa za nyuklia ni mambo ambayo yanafuatiliwa kwa hima na uzito mkubwa nchini Iran.  

Katika sehemu moja ya ujumbe wake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia, Dk Salehi amesema, suala la kuzidishwa sana uzalishaji na huduma zinazohusiana na sekta ya matibabu yanayotumia teknolojia ya nyuklia na kuvidhaminia  mahitaji ya dawa vituo vya tiba na afya nchini Iran kunafanyika kwa kiwango cha juu na kwa kasi inayokubalika.

Dk Ali Akbar Salehi

 

Mradi wa nyuklia wa Iran unaotumia uwezo wa ndani na uliojikita kwenye kufanikisha malengo maalumu yaliyoainishwa tangu zamani, unaendelezwa katika mihimili minne mikuu ambayo ni pamoja na kukamilishwa mchakato wa uzalishaji wa fueli nyuklia, kupata teknolojia za kisasa, kuzalisha nishati na nne kutumia nunurishi katika kazi za kilimo, viwanda na matibabu ambapo leo hii Iran imepata mafanikio makubwa katika nyuga zote hizo.

Katika elimu ya nyuklia, mchakato kamili wa uzalishaji wa fueli nyuklia unahitajia kuwa na teknolojia ya hali ya juu sana na Iran imefanikiwa kuzalisha asilimia 20 ya fueli nyuklia katika kipindi kifupi sana na kuwaonesha walimwengu uwezo wake mkubwa wa kielimu. Vifaa vilivyozalishwa na Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran ndivyo vinavyotumika hivi sasa katika kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran.

Sehemu nyingine muhimu ya faida za teknolojia ya nyuklia ni upande wa tiba na matibabu. Matibabu kama ya mionzi ni muhimu sana kwenye sekta ya afya na hayo ni katika mafanikio makubwa iliyopata Iran kwenye mradi wake wa nyuklia wa matumizi ya kiraia. 

Tarehe 8 Aprili ni siku ambayo Iran ilipata mafanikio makubwa katika mradi wake wa nyuklia. Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika masuala ya nyuklia kwa kutegemea wataalamu wao wa ndani. Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza wazi kuwa iko tayari kuyapa mataifa mengine uzoefu wake katika uwanja huo.

Kinu cha nyuklia cha Bushehr, nchini Iran

 

Licha ya kupata teknolojia hiyo kubwa chini ya mashinikizo ya pande zote ya maadui, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema haina kinyongo na mtu na itaendelea kuhesimu kikamilifu makubaliano yote ya nyuklia na itaendelea kuruhusu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuchukunguza kwa karibu miradi yake mbalimbali kwani ni ya amani kikamilifu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuwa akilisisitizia sana suala hilo. Katika sehemu moja ya miongozo yake ya busara aliyoitoa wakati alipoonana na watu wenye vipaji mbalimbali vya kielimu nchini Iran mwaka mmoja uliopita alisema: Kama elimu itatenganishwa na njia yake sahihi, hufanya makosa. Licha ya kwamba elimu ya nyuklia ina manufaa lakini kwa vile haikutumika kwenye kuhudumia wanadamu, imepotea njia na kuzalisha bomu la nyuklia na hadi hivi sasa ni tishio kwa usalama wa dunia nzima. Sisi licha ya kwamba tungeliweza kufanya hivyo lakini tulisimama imara na kishujaa na hatukwenda upande huo wa kuzalisha silaha za nyuklia. Sisi tunaamini kuwa, kuzalisha bomu la nyuklia ni kosa na kujilimbikizia mabomu hayo pia ni kosa kwani ni haramu kutumia silaha hizo.

Kwa mtazamo huo tunaweza kusema kukwa, ustawi uliopatikana humu nchini katika teknolojia ya nyuklia na mafanikio yake makubwa ni nembo ya nguvu na fakhari ya kitaifa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Maoni