Apr 08, 2020 13:16 UTC
  • Rais wa Iran azitaka IMF na Benki ya Dunia kutekeleza majukumu yake ipasavyo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia zinapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwamba, katika mazingira magumu ya sasa kama hayatotekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa, basi walimwengu watakuwa na ufahamu na uelewa mwingine kuhusiana na jambo hilo.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri na kueleza kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Iran haijawahi kuomba msaada wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na kutahadharisha kwamba, endapo IMF itafanya ubaguzi baina yan Iran na mataifa mengine, jambo hilo katu halitakubalika.

Raiswa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha utendaji wa upande mmoja wa Marekani na kueleza kwamba, daima serikali ya Washington imekuwa na undumakuwili huo na katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona pia, dola hilo la kibeberu linaendeleza utendaji huo ghalati pamnoja na fikra hiyo isiyo sahihi.

Dakta Hassan Rouhani amebainisha pia kuwa mbali na Marekani kuendesha ugaidi wa kiuchumi, imekuwa ikitekeleza pia ugaidi katika sekta ya tiba.

Aidha amesema, kuhusiana na kadhia ya Corona, Marekani imekiuka wazi wazi azimio la mwaka 2005 la Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linahimiza mataifa yote kushirikiana kwa ajili ya kukabiliana na maradhi ya kuambukiza.

Raisw a Iran amesema kinagaubaga kwamba, doa hili jeusi la kihistoria litabakia kwa mapaji ya uso ya watawala wa serikali ya Marekani ambao hata katika mazingira haya magumu, wangali wanaendeleza mashinikizo yao dhidi ya taifa hili.

Maoni