Apr 09, 2020 13:11 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Hitajio la mwanadamu wa leo kwa mkombozi ni nadra kuwahi kushuhudiwa katika historia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hitajio la kina na pana la mwanadamu wa leo la kuwa na mkombozi ni nadra kushuhudiwa katika historia. Amesisitiza kuwa, maana halisi na yenye manufaa ya kusubiri mwokozi ni kuwa na matumaini na itikadi kuhusu faraja sambamba na kuchukua hatua za kufikia mustakbali mwema na akaongeza kuwa: "Taifa la Iran limefaulu vizuri katika mtihani wa ugonjwa wa hivi karibuni; na mwenendo na nidhamu ya umma ni nzuri katika kufuata maelekezo."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Alhamisi mjini Tehran katika hotuba ya kitaifa ya moja kwa moja kwa njia ya televisheni kwa Mnasaba wa Shaaban 15, siku ya kukumbuka kuzaliwa Qaim Aal Muhammad yaani Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake).  Kiongozi Muadhamu ametuma salamu zake za pongezi kwa taifa la Iran, Waislamu na wapendao uhuru kote duniani kwa munasaba huu adhimu wa kukumbuka kuzaliwa Waliul Asr, yaani Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake). Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, sayansi, hekima na jarabati ni kati ya neema kubwa za Mwenyezi Mungu na huweza kutatua matatizo mengi lakini akaongeza kuwa: "Hata hivyo, na kama ambavyo imethibitika hadi sasa, sayansi na hekima haziwezi kutatua tatizo la ukosefu wa uadilifu na ili kufikia tamanio hilo kubwa la mwanadamu inahitajika nguvu ya Mwenyezi Mungu na ni kwa sababu hii ndio jukumu hili kubwa akakabdihiwa Hadhrat Baqiyatullah Al Aadham (Imam Mahdi) ili aweze kuijaza ardhi haki na uadilifu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hali iliyotokana na ugonjwa wa corona duniani na kusema kadhia hii ni mtihani  jumla na wa ajabu kwa mataifa na serikali na kuongeza kuwa: "Kusubiri faraja kuna maana ya kupata ahueni baada ya shida na kwa sababu hii, mwanadamu mwenye kusubiri hapotezi matumaini au kuchanganyikiwa kutokana na tukio hili na anadumisha utulivu wake kwa sababu anajua bila shaka hali itabadilika."

Kiongozi Muadhamu amekumbusha kuhusu utendaji wa nchi za magharibi kuhusu kadhia ya corona na akaashiria mfano wa uporaji maski na glavu unaofanywa na baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, namna watu  walivyovamia kwa fujo maduka makubwa na kuhatarisha maisha yao wakipigania karatasi laini za chooni, pia watu kupanga foleni kwa ajili ya kununua silaha, na vile vile kutotibiwa wazee sambamba na kujiua watu, kuwa ni mambo yanayotokana na hofu ya corona. Amesema matukio hayo yanaonyesha wazi natija iliyotarajiwa ya utamaduni na ustaarabu wa nchi za Magharibi ambao umejengeka juu ya msingi wa Ubinafsi (Individualism), Umaada (Materialism) na kutawaliwa zaidi na kutomuamini Mwenyezi Mungu (Atheism). 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vita vikuu vya kwanza na vya pili va dunia, vita vya Vietnam na hujuma za Marekani katika nchi za Afghanistan na Iraq ni kati ya matukio muhimu ya miaka iliyopita na kuongeza kuwa: "Janga la corona lisitufanye tukaghafilika na dhulma na ukandamizaji wa madola makubwa ya dunia kwa mataifa mbali mbali yakiwemo mataifa ya Palestina na Yemen." Aidha amesema hatupaswi kughafilika na njama na uadui wa uistikbari wa kimataifa, kwani kinyume na wanavyodhani baadhi, ambao wanasema tusipofanya uadui, wao pia hawatakuwa na uadui na sisi, uistikbari  una uadui na mfumo wenyewe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi.

Tags

Maoni