Apr 09, 2020 13:16 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; kung’ara taifa la Iran katika mtihani wa virusi vya Corona

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, taifa la Iran limeng’ara na kufaulu vizuri katika mtihani mgumu wa virusi vya Corona, hata hivyo kilele cha fahari ni mali ya wafanyakazi wa sekta ya tiba na afya.

Ayatullah Syyid Ali Khamenei amesema hayo katika hotuba yake aliyotoa mubashara leo kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu Imam Mahdi (atfs) iliayoadhimishwa hii leo hapa nchini Iran na katika ulimwengu wa Kiislamu, ambapo mbali na kuutaja ushiriki wa wananchi katika maeneo yote ya Iran kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa Corona na wahitaji kwamba, ni wa kushangaza amesisitiza kuwa, harakati zote hizi zenye thamani ni ishara ya wazi ya kukita mizizi utamaduni wa Kiislamu baina ya wananchi.

Baada ya virusi vya Corona kuingia hapa nchini Iran, jamii ya madaktari na wauguzi ilijitokeza na kuwa katika mstari wa mbele katika kupambana na virusi hivi angamizi. Aidha matabaka mengine ya wananchi nayo yakitegemea utamaduni mkubwa wa urafiki na kuishi pamoja nayo yaliingia katika medani hii ya vita dhidi ya virusi vya Corona.

 

Kipindi hiki cha kuweko virusi vya Corona nchini Iran kwa hakika ni siku za kilele cha kudhihirika udugu na urafiki wa kibinadamu, huba na mapenzi baina ya watu ambao hawatelekezani na kutupana mikono katika mazingira magumu ambapo hivi sasa wanatumia mbinu mbalimbali tena usiku na mchana kwa ajili ya kupambana na maradhi haya.

Vijana, vikundi vya kujitolea vya hima na jihadi, basiji, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Jeshi la Iran wote hawa wakiwa bega kwa bega na timu za madkatari na wauguzi wanatumia nguvu zao zote ili kupitia utamaduni wa Kiirani-Kiislamu waweze kuviangamiza haraka virusi hivi vya Corona.

Kuzalishwa kwa wingi tena na wananchi wa kawaida vitu kama barakoa (maski) na vitakasa mikono nchini Iran na vifaa hivyo kugawiwa bure baina ya wananchi hususan matabaka ya wananchi wenye kipato cha chini na kuanzishwa na jeshi la Iran vituo na hospitali kwa ajili ya kutoa tiba na huduma kwa waathirika wa virusi vya Corona na kubwa zaidi kuweko himaya ya kimaanawi kwa madaktari na wauguzi, ni sehemu tu ya kazi nyingi za kibinadamu zinazoshuhudiwa katika kipindi hiki kigumu baina ya wananchi wa taifa hili.

 

Tukilinganisha muamala na moyo wa wananchi, madaktari na wauguzi wa Iran na ile anga inayotawala katika jamii ya Wamagharibi iliyojengeka juu ya misingi ya falsafa na utamaduni wa Kimagharibi tunaelewa wazi ni jinsi gani utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu ulivyokuwa na taathira nzuri kwa wananchi wa taifa hili la Kiislamu. Nchini Iran watu wote wanafanya hima kwa pamoja kwa ajili ya kulinda uhai na roho za watu huku katika utamaduni na falsafa ya Kimagharibi tunashuhudia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi na madaktari ambavyo kwa hakika vinakinzana wazi na utu pamoja na ubinadamu.

Katika uwanja huo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mifano ya wazi kama kuporwa maski na glovu za mataifa mengine kulikofanywa na baadhi ya madola ya Ulaya na Marekani, kupanga safu watu kwa ajili ya kununua silaha, kutotibiwa wagonjwa ambao ni wazee na kujiua watu kutokana na hofu ya virusi vya Corona na kusema kuwa: Katika matukio haya, utamaduni na ustaarabu wa Magharibi umedhihirisha wazi mazao yake ambapo haya ni matunda ya kawaida kabisa kwa falsafa inayotawala katika utamaduni wa Kimagharibi uliojengeka juu ya misingi ya ubinafsi, kufadhilisha mambo ya kimaada na ambao aghlabu haumtambui Mwenyezi Mungu.

Vifurushi vya maski za China kwa ajili ya Ujerumani

 

Baadhi ya vitendo vya wananchi na madola ya Magharibi katika siku hizi vimeonyesha kuwa, ustaarabu wa Kimagharibi hauna thamani, utambulisho na urafiki wa kibinadamu na utendaji wa aina hii umekabiliwa na radiamali ya baadhi ya shakhsia hata ndani ya Magharibi kwenyewe.

Andreas Geisel, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani ameashiria kuporowa na Marekani kifushi cha maski 200,000 kilichokuwa kikitokea China na kusema kuwa, hatua hiyo ni uharamia wa kisasa. Sambamba na kulaani kitendo hicho cha serikali ya Marekani amewahutubu Wamarekani na kusema kuwa, hata kama kuna mgogoro wa kimataifa lakini hakupaswi kutumiwa mbinu za magenge katili ya zamani ya Kimagharibi.

Kwa hakika hii ni sehemu ndogo tu ya mifano ya miamala na vitendo vinavyotawala katika ustaarabu wa Magharibi, ambao unadai kuwa umeendelea na kupiga hatua katika nyanja zote, lakini kama alivyosema Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa, tukitupia jicho jamii hizi mbili yaani jamii ya Kiislamu na ya Magharibi katika kipindi hiki cha mtihani wa virusi vya Corona, tunaona kuwa, serikali ya Iran na wananchi wa taifa hili  wameng’ara na kufaulu vizuri mtihani huu kutokana na kuonyesha kwao  mwenendo na utendaji wa kiutu na kibinadamu katika nyuga zote za kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kusaidiana baina yao; na ustawi na maendeleo katika ustaarabu wa Kiislamu maana yake ni uenezaji wa kweli wa uadilifu na umaanawi katika jamii.

Tags

Maoni