Apr 10, 2020 12:01 UTC
  • Zaidi ya watu 35,000 wapata afueni ya corona nchini Iran

Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Matibabu ya Iran imetangaza kuwa, kasi ya mchakato wa kuzidi kupata afya njema na afueni kutokana na Corona imeongezeka sana humu nchini kiasi kwamba, hadi leo mchana watu 35 elfu na 465 walisharuhusiwa kurudi nyumbani kutoka mahospitalini baada ya kupata nafuu kikamilifu.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza habari hiyo leo mbele ya waandishi wa habari na kueleza kwamba, mwenendo wa kupona watu waliokuwa wameathiriwa na virusi vya Corona umeongezeka mno hapa nchini jambo ambalo linatia matumaini.

Aidha amesema kuwa, watu wapatao 1,972 wameambukizwa virusi vya Corona katika masaa 24 yaliyopita na kufanya idadi ya walioambukizwa virusi hivyo hadi sasa hapa nchini Iran kufikia 68,192.

Daktari Jahanpour amesema pia kuwa, idadi ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita humu nchini ni watu 122, na kuifanya idadi ya waliopoteza maisha nchini Iran kutokana na ugonjwa huo hadi hivi sasa kufikiawatu 4,232.

Virusi vya Corona ambavyo vilianzia katika mji wa Wuhan China, hivi sasa vimeenea karibu kote duniani ambapo hadi kufikia leo mchana, watu milioni moja, laki sita na 17 elfu na 576 (1,617,576) walikuwa wameshathibitishwa kukumbwa na Corona kote ulimwenguni.

Huku kila nchi ikifanya juhudi za kukabiliana na virusi vya Corona, taathira za janga hili hasa katika sekta ya uchumi zimeanza kuoneka.

Baadhi ya mashirika yamelazimika kuwapunguza wafanyakazi au kuwapa likizo bila malipo kutokana na hasara yanayopata kufuatia kusimama sehemu kubwa ya shughuli zake kutokana na mlipuko wa virusi hivi angamizi.

Maoni