May 02, 2020 07:52 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuwanufaisha wengine uzoefu tuliopata wa kukabiliana na corona

Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuyanufaisha mataifa mengine uzoefu wake katika suala la kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri amesema hayo leo Jumamosi katika ujumbe mbalimbali aliowatumia  kwa nyakati tofauti Mawaziri wa Ulinzi na Wakuu wa Komandi za Vikosi vya Ulinzi wa nchi za Iraq, Jamhuri ya Azerbaijan, Afghanistan, Pakistan, Oman, Qatar, Kuwait, Syria na Lebanon na huku akigusia mafanikio makubwa iliyopata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na maambukizi ya corona, amezungumzia pia mchango mkubwa wa vikosi vya ulinzi humu nchini katika kukabiliana na kirusi hatari cha corona. Amesema, vikosi vya ulinzi vya Iran viko tayari kuzipatia nchi rafiki uzoefu vilioupata katika kupambana na ugonjwa huo. 

Vita dhidi ya corona nchini Iran

 

Mkuu huyo wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran amesisitiza kuwa, kutopambana kwa njia sahihi na kiutalaamu na ugonjwa wa corona kunaweza kuongeza kasi ya kuenea ugonjwa huo na kuutia hatarini usalama wa taifa zima. Ameongeza kuwa, mafanikio iliyopata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na kuudhibiti ugonjwa wa COVID-19 ni fursa nzuri kwa mataifa mengine ya Kiislamu na nchi marafiki na jirani na Iran, ya kuweza kupambana vilivyo na ugonjwa huo.

Ugonjwa wa corona ambao jina lake rasmi na COVID-19 uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan, China, mwishoni mwa mwaka 2019 na hivi sasa umeshaenea katika nchi zote duniani. Idadi ya watu waliokuwa wameshaambukizwa corona kote duniani kufikia leo asubuhi ilikuwa ni 3,402,034 (milioni tatu na laki nne na elfu na 34). Kati ya hao watu 1,083,908 (milioni moja na 83 elfu na 908) walikuwa wameshapona na 239,622 walikuwa wameshafariki dunia kufikia leo asubuhi.

Tags