May 21, 2020 07:52 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Tutaliunga mkono taifa lolote linalopambana na utawala wa Kizayuni

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italiunga mkono taifa lolote lile linalosimama kidete dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

 Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika ujumbe uliotumwa kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Tutaliuga mkono na kulisaidia taifa na kundi lolote lile na popote pale linaloupinga na kulipiga vita utawala wa Kizayuni, na hatutasita kuyasema haya.

Amesema mapambano jumuishi ya taifa la Palestina, kisiasa, kijeshi na kiutamaduni yanapaswa kuendelea hadi pale maghasibu watakapoafiki maoni na msimamo wa Wapalestina. Ameongeza kuwa, "taifa hili (la Palestina) linapaswa kujiamulia lenyewe mfumo wa kisiasa unaopaswa kuliongoza, na mapambano lazima yaendelee hadi wakati huo."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameeleza bayana kuwa, "kuung'oa utawala wa Kizayuni hakuna maana ya kuwaung'oa Mayahudi, sisi hatupo dhidi ya Mayahudi, lakini kunamaanisha kuung'oa utawala pandikizi; na Waislamu, Wakristo Wapalestina Mayahudi waachwe wachague serikali waitakayo, na kuwafukuza majambazi kama Netanyahu. Huku ndiko kuing'oa Israel, na litafanyika."

Baadhi ya shakhsia wa kimataifa wanaotazamiwa kutoa hotuba kwa njia ya mitandano kwa mnasaba wa Siku ya Quds

Amekumbusha kuwa, pendekezo la Iran la kufanyika kura ya maoni ya Wapalestina kuchagua serikali wanayoitaka limesajiliwa katika Umoja wa Mataifa. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anatazamiwa kesho Ijumaa kutoa hotuba yake kwa njia ya video kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds. Hotuba hiyo itakayoanza saa sita adhuhuri kwa saa za hapa nchini Iran itapeperushwa hewani mubashara na radio na televisheni za ndani na nje ya Iran, na pia katika mitandao ya kijamii.

 

Tags

Maoni