May 23, 2020 02:38 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kuhusu kukaribia kuangamia utawala wa Kizayuni katika eneo

"Bila shaka kirusi cha Uzayuni hakitadumu kwa muda mrefu na kwa kutegemea hima, imani, ghera ya vijana, mizizi ya kirusi hicho itang'olewa na kuondolewa katika eneo".

Hiyo ni kauli ya Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipozungumza kwa njia ya televisheni Ijumaa adhuhuri kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amebainisha ukweli huo kuhusu kuangamia utawala wa Kizayuni sambamba na kuwasilisha uchambuzi kamili kuhusu matukio ya eneo ambapo amewasilisha nasaha saba muhimu kuhusu kuendelea jihadi kubwa na takatifu ya hivi sasa.

Nasaha hizo saba muhimu za Ayatullah Khamenei katika hotuba yake ya Siku ya Kimatiafa ya Quds ni pamoja na: “Kutoifanya kadhia ya Palestina kuwa kadhia ya Wapalestina au Waarabu tu”, “kukombolewa ardhi zote za Palestina kutoka bahari hadi mto na kurejea Wapalestina  wote katika ardhi zao”, “kujizuia kuyaamini madola makubwa ya kidhalimu ya Magharibi, taasisi tegemezi za kimataifa na baadhi ya serikali vibaraka katika eneo,” “vijana wenye ghera katika ulimwengu wa Kiislamu wafuatilie matakwa ya kukabiliana na njama za Wamarekani na Wazayuni”, “kukabiliana na hali mbaya na yenye madhara ya uwepo wa Wamarekani na Wazayuni”, “kuendeleza mapambano na kupanua wigo wa Jihadi katika ardhi za Palestina” na  “kufanyika kura ya maoni yenye kuwajumuisha Wapalestina wa dini na kaumu zote.”

Hotuba na nasaha za Kiongozi Muadhamu kuhusu kadhia ya Palestina zimejikita katika masuala mawili muhimu na ya kistratijia ambapo katika upande mmoja amewahutubu viongozi wa kisisia katika ulimwengu wa Kiislamu na katika upande wa pili ni kuhusu kufikia haki za taifa linalodhulimuwa la Palestina.

Maandamano ya Siku ya Kimatiafa ya Quds nchini Tanzania miaka iliyopita

Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu; msimu mpya katika kupigania ukombozi wa Palestina ulianza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 na leo, kwa hima na irada ya mrengo wa muqawama au mapambano,  tunashuhudia kubadilika mlingano wa nguvu kwa maslahi ya wanamapambano.

Pamoja na hayo, kuna baadhi ya mienendo inayoshuhudiwa ambayo ni ya wale wanaotaka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Hii ni mienendo ambayo haijakuwa na natija nyingine yoyote ghairi ya kujisalimisha mbele ya mashinikizo na udhalilishaji wa Marekani, Ulaya na Israel.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema natija ya kujisalimsha huku ni kupotosha mkondo wa mapambano na kuupeleka katika mazungumzo yasiyo na faida na Wazayuni maghasibu na waungaji mkono wao. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: “Ni katika mazingra kama hayo ndipo yakadhihiri Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na hivyo msimu mpya ukaanza katika mapambano ya Palestina. Baada ya kujitokeza mrengo wa muqawama na mapambano, hali ya utawala wa Kizayuni imekuwa ngumu na bila shaka hali itazidi kuwa ngumu katika mustakabali.”

Tokea kuasisiwa kwake mwaka 1948, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifuatilia malengo mawili.

Lengo la kwanza; ni kujaribu kupata uhalali sambamba na kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Lengo hilo halijaweza kufikiwa kwa sababu Wapalestina wanatekeleza mapambano na muqawama na hivyo kuuweka katika changamoto kubwa uhalali wa utawala bandia wa Israel.

Lengo la pili; ni kuudhibiti na kuukalia kwa mabavu mji wa Quds au Baitul Maqdis (Jerusalem), ambao ndiko kuliko kibla cha kwanza cha Waislamu. Utawala wa Israel unafuatilia lengo la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Quds Tukufu.

Ni kwa msingi huo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akatoa nasaha za kistratijia zenye kusisitiza  kuendelea na mapambano katika uga wa jihadi katika maeneo yote ya Palestina.

Hakuna shaka kuwa, haki ya kurejea Wapalestina waliotimuliwa kutoka ardhi zao za jadi, na haki yao ya kuainisha hatima yao na pia haki ya kuunda serikali huru ya Palestina ni misingi mikuu ya haki za taifa la Palestina katika fremu ya sheria za kimataifa. Ni kwa kuzingatia misingi hiyo ndio, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nasaha zake akasisitiza kuwa, Palestina ni ya Wapalestina wote na kwamba inapaswa kuendeshwa kwa irada yao. Kiongozi Muadhamu kwa mara nyingine amewasilisha mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kufanyika kura ya maoni yenye kuwahusisha Wapalestina wa dini na kaumu zote na kusema: “Mpango huu unaonyesha kuwa, madai ya chuki dhidi ya Uyahudi, ambayo yanakaririwa katika vyombo vya habari vya Kimagharibi hayana msingi wowote.”

Katika hotuba yake ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Kiongozi Muadhamu ameashiria pia ukweli mwingine na kusema: “Kile ambacho bila  shaka lazima kiangamie ni mfumo wa Kizayuni na Uzayuni.”

 

Tags

Maoni