May 23, 2020 07:54 UTC
  • Iran yatoa mkono wa pole kufuatia ajali ya ndege ya Pakistan iliyoua 97

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pole kwa serikali na raia wa Pakistan kufuatia ajali ya ndege ya abiria ya nchi hiyo iliyoua makumi ya watu.

Rais Rouhani ameonyesha masikitiko yake kufuatia ajali hiyo ya ndege ya Pakistan na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa tukio hilo la jana Ijumaa, katika ujumbe aliomtumia Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Imran Khan.

Serikali ya Pakistan imetangaza kwamba watu 97 waliokuwepo kwenye ndege hiyo ya abiria walipoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea karibu na uwanja wa ndege ulioko katika mji wa bandari wa Karachi.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Pakistan, Meeran Yousuf amesema abiria wawili wa kiume wamenusurika kwenye ajali hiyo iliyohusisha ndege ya abiria yenye nambari ya usajili PK-8303, iliyokuwa ikitokea mji wa mashariki wa Lahore kuelekea Karachi.

Sehemu ilikoandika ndege ya Pakistan

Kadhalika watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya ndege hiyo kuangukia nyumba zao katika ajali hiyo ya jana. Kwa akali nyumba tano zimeteketea kwa moto kikamilifu kufuatia ajali hiyo.

Chanzo cha ajali hiyo hakijatangazwa hadi sasa, lakini vyombo vya dola vya Pakistan vimeanzisha uchunguzi kubaini kiini chake.

 

Tags

Maoni