May 24, 2020 07:40 UTC
  • Swala ya Idi yaswaliwa katika misikiti nchini Iran

Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo wameshiriki katika swala ya Idul Fitr baada ya kukamilisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Ofisi ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana ilitoa taarifa na kusema, leo, Jumapili ni  tarehe Mosi Shawwal na siku kuu ya Idul Fitr.

Kwa mujibu wa maamuzi ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na COVID-19, kulikuwa na idhini ya kuswali swala ya Idul Fitr katika miji yote. Hata hivyo kwa mujibu wa maelekezo ya idara hiyo hakukuwa na swala katika viwanja vikubwa bali watu wamejimuika makundi madogo madogo katika misikiti na viwanja au mabustani mitaani ambapo waumini walioshiriki katika swala wamezingatia kanuni ya kutokaribiana na kuvaa barakoa. 

Waumini katika Swala ya Idi mjini Tehran

Kwa kawaida Swala ya Idi huswaliwa mjini Tehran katika Uwanja wa Swala wa Imam Khomeini  ambao una uwezo wa kubeba malaki ya waumini lakini mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 wakuu wa afya nchini Iran wameshauri kuwa waumini wasijumuike katika eneo hilo. 

Leo katika aghalabu ya nchi za Kiislamu ni siku kuu ya Idul Fitr.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia viongozi wa nchi za Kiislamu na Waislamu kote duniani salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia siku kuu ya Idul Fitr.

Maoni