May 24, 2020 10:46 UTC
  • Brig. Jen. Hajizadeh: Utayarifu wa kujihami Iran upo katika kiwango cha juu zaidi

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kuwa, utayarifu wa kulihami na kulilinda wa taifa la Iran hivi sasa upo katika kiwango cha juu zaidi katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amesema hayo leo Jumapili katika mahojiano aliyofanyiwa pambizoni mwa Swala ya Idul-Fitr na kuongeza kuwa, "hivi sasa, sekta ya uchumi ndilo jambo linalopaswa kupewa mazingatio makubwa."

Amesema wasi wasi kuhusu uwezo wa kiulinzi wa Iran hauna msingi wowote na ni njama za maadui za kujaribu kupotosha na kulivuruga taifa la Iran. Amesisitiza kuwa: Tunamshukuru Allah, Iran ni taifa kubwa na lenye uwezo mkubwa na hili linawatia kiwewe maadui.

Brigedia Jenerali Hajizadeh amesema kuwa, katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliwa na hujuma za kila namna za maadui na kusisitiza kuwa, usalama na ulinzi wa taifa hili ni vipaumbele vikuu vya vikosi vya ulinzi vya Iran.

Aina za makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Hapo jana Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa taarifa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kukombolewa mji wa Khoram-Shahr ulioko kusini magharibi mwa Iran mnamo mwaka 1982 na kueleza bayana kuwa: leo hii Jamhuri ya Kiislamu imepiga hatua kubwa ya kujitosheleza katika uga wa ulinzi, na hii ni stratejia ya ushindi iliyochukuliwa na Iran dhidi ya madola ya kibeberu.

Tags

Maoni