May 25, 2020 12:13 UTC
  • Larijani: Kukombolewa kusini mwa Lebanon ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa Asia Magharibi

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, kukombolewa kusini mwa Lebanon ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa na muhimu katika eneo la Asia Magharibi mabadiliko ambayo kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu yataishia kwenye kukombolewa Quds na ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Dk Ali Larijani alisema hayo jana katika ujumbe aliomtumia Nabih Beri, Spika wa Bunge la Lebanon kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa kukombolewa kusini mwa Lebanon kutoka katika makucha katili ya utawala vamizi wa Israel. 

Amesema, ni jambo lisilo na shaka kwamba tukio hilo kubwa ni kito chenye thamani kubwa katika historia ya mapambano ya wananchi wa eneo hili dhidi ya utawala pandikizi wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu. Kufurushwa Wazayuni hao huko kusini mwa Lebanon kulisambaratisha ile ngano kwamba eti Israel haishindiki na tangu wakati huo hadi hivi sasa kambi ya muqawama imekuwa ikipata ushindi mtawalia dhidi ya Wazayuni.

Wanamapambano wa Lebanon wakisherehekea ushindi wakati walipowafurusha wanajeshi Wazayuni kusini mwa nchi yao

 

Itakumbukwa kuwa tarehe 25 Mei 2000, utawala wa Kizayuni wa Israel ulikimbia kwa madhila kusini mwa Lebanon na licha ya kuwa na uwezo wa kijeshi, lakini ilishindwa kukabiliana na wanamapambano wa Kiislamu.

Kila mwaka wananchi wa Lebanon wanaiadhimisha kwa sherehe siku hiyo ambayo wanaitambua kuwa ni siku ya ushindi na muqawama.

Tags

Maoni