May 30, 2020 04:18 UTC
  • Spika mpya wa Bunge la Iran ahimiza umoja wa Waislamu dhidi ya Israel

Spika mpya wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amesisitizia umuhimu wa umoja wa Waislamu na jitihada za pamoja za kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mohammad Baqer Qalibaf ametoa mwito huo katika mazungumzo yake ya simu na Spika wa Bunge la Uturuki, Mustafa Sentop ambapo wamezungumzia matukio ya eneo hili la Asia Magharibi.

Amesema mataifa ya Kiislamu yanapaswa kushirikiana na kuunganisha nguvu zao ili yaweza kuzima njama chafu zinazopangwa na utawala haramu wa Israel, hususan dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Kadhalika Qalibaf amesema kuna udharura kwa Iran na Uturuki kuimarisha ushirikiano wao katika kuhakikisha kunakuwepo na amani na usalama wa kudumu katika eneo.

Spika mpya wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Uturuki daima zimekuwa na uhusiano wa kirafiki ambao upo katika kiwango cha juu kabisa. Kuna haja ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi baina ya Ankara na Tehran na karibuni hivi, Bunge jipya la Iran litaunda kundi la urafiki baina ya nchi hii na Uturuki."

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika mpya wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu

Aidha ametoa mwito wa kuendelezwa mazungumzo ya pande tatu baina ya Iran, Uturuki na Russia katika fremu ya Astana, ya mchakato wa amani ya Syria.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Uturuki, Mustafa Sentop sambamba na kumpongeza Mohammad Baqer Qalibaf kuchaguliwa kuwa Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema Bunge la Uturuki lipo tayari kuimarisha uhusiano wa kibunge baina ya mataifa haya mawili. Ameongeza kuwa, nchi hiyo ina hamu ya kuimarisha uhusiao wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na kusisitiza kuwa, "natumai nchi mbili hizi jirani zitarejesha uhusiano wao wa kibiashara katika kiwango cha huko nyuma cha kabla ya janga la corona."

 

Tags

Maoni