Jun 02, 2020 03:58 UTC
  • Vitisho vya Marekani dhidi ya dunia kwa mtazamo wa Katibu Mkuu wa Idara ya Haki za Binaadamu ya vyombo vya Mahakama vya Iran

Hivi sasa walimwengu wamebainikiwa kwamba vitisho vya Marekani havikomei tu kwa viongozi wa nchi hiyo, bali ni mfumo wa kifikra uliokita mizizi katika muundo wa uongozi wa nchi hiyo.

Ali Bagheri Kani, Katibu Mkuu wa Idara ya Haki za Binaadamu ya vyombo vya Mahakama nchini Iran ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya pili ya televisheni ya Iran ambapo akiashiria ukweli huo, amesema kuwa ni lazima zichukuliwe hatua za kuzuia kuenea mfumo huo wa kifikra duniani. Kwa sasa raia wa Marekani wamechoshwa na ubaguzi wa rangi, ufisadi, dhulma na uongozi duni wa viongozi wa nchi yao, na hii leo dunia nzima inasikia kilio chao. Hivi sasa kunashuhudiwa maandamano na malalamiko makubwa ya Wamarekani. Malalamiko ambayo mara hii pia yameibuka kufuatia mauaji ya kutisha dhidi ya Mmarekani mweusi. Ni vyema kuashiria kuwa Jumatatu ya wiki jana afisa mmoja wa polisi mzungu alimuua kinyama Mmarekani mweusi George Floyd katika mji wa Minneapolis, jimboni Minnesota. Rais Donald Trump amewataja waandamanaji weusi wanaopinga mauaji hayo kuwa ni majambazi na kutishia kwamba polisi na majeshi ya Marekani yatawafyatulia risasi hai.

Ali Bagheri Kani, Katibu Mkuu wa Idara ya Haki za Binaadamu ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran

Maandamano hayo ya kulaani hatua na vitendo vya mabavu vya polisi vilivyo dhidi ya ubinaadamu, sio ya kueneza ukatili, bali ni ya kukabiliana na ukatili. Kwa mujibu wa Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ili kuwatisha waandamanaji Marekani inatumia jeshi, mbwa wakali na silaha za moto. Badala ya kutumia mbinu hizo za ukandamizaji, Marekani inatakiwa kusikiliza sauti ya wananchi wake na kubadilisha siasa zake zilizofeli katika kuamiliana nao. Matamshi ya Katibu Mkuu wa Iara ya Haki za Binaadamu ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran pamoja na ya jumbe za Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hii yameweka wazi uhalisia wa fikra na makelele yaliyoratibiwa katika muundo wa siasa na utawala wa Marekani nyuma ya nara za hadaa kama vile za eti kutetea uhuru na demokrasia na haki za binaadamu. Ni vyema kuashiria kuwa, Marekani ndio nchi inayoongoza duniani kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu kama ambavyo pia inaunga mkono tawala zinazoua watoto na wanawake kama vile utawala haramu wa Israel na Saudi Arabia. Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazodai kuwa ni watetezi wa haki za binaadamu, ziliupatia utawala wa Saddam wa Iraq silaha za kemikali zilizotumika dhidi ya raia wa Iran na kuwafanya wahanga zaidi ya watu laki moja.

Polisi wa Marekani wametakiwa kuwashambulia kwa risasi hai waandamanaji bila huruma

Aidha Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, zimekuwa zikiliunga mkono kundi la kigaidi la Munafiqin (MKO) ambalo mikono yake imetapakaa damu za Wairani wasio na hatia elfu 17. Hivi sasa Marekani katika kipindi hiki cha kuenea virusi hatari vya Corona, imetia rekodi mpya ya ukandamizaji wa haki za binaadamu. Kupitia vikwazo vyake vya madawa na vifaa vya tiba, Marekani imeyalenga moja kwa moja maisha ya Wairani. Mambo yote hayo yanaonyesha kwamba adui mkubwa wa haki za binaadamu na demokrasia, ni wale wanaotumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa siasa za nje dhidi ya mataifa na serikali halali za nchi tofauti zinazopinga ubeberu wao. Kuhusiana na suala hilo Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Marekani kuwa nchi inayoongoza duniani kwa ukiukaji wa haki za binaadamu, na kubainisha kwamba, watu ambao wanamiliki jela za kuogofya kama vile za Guantanamo na Abu Ghraib sambamba na kushambulia maeneo ya makazi ya raia nchini Iraq, Afghanistan na maeneo mengine, hawafai kutoa madai ya kuteta haki za binaadamu, wala hata kuzungumzia suala hilo kwa sababu wao ndio wakiukaji wakubwa wa haki za binaadamu ulimwenguni.

Maoni