Jun 02, 2020 08:16 UTC
  • Iran: Viashiria vya kusambaratika Marekani vinazidi kudhihiri

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusiana na maandamano yanayoendelea nchini Marekani kufuatia kuuawa kinyama na polisi mzungu Mmarekani mwenye asili ya Afrika na pia kitendo cha Trump kujificha chini ya White House kwa kuogopa hasira ya waandamanaji.

Katika ujumbe huo Shamkhani amesema kuwa matukio hayo yanabainisha viashiria zaidi vya kusambaratika 'shetani mkubwa' yaani Marekani. Hii ni katika hali ambayo miji tofauti ya Marekani hususan mji wa Minneapolis katika jimbo la Minnesota imekuwa ulingo wa maandamano ya wananchi wanaolaani mienendo ya kibaguzi ya polisi wa nchi hiyo. Baada ya polisi mzungu kumuua kinyama George Floyd, Mmarekani mweusi raia wa Marekani raia wa nchi hiyo wamejawa na hasira na kumiminika barabarani kulaani jinai hiyo.

Ghasia zinazoendelea nchini Marekani

Hata hivyo Rais Donald Trump ametoa amri kwa jeshi la polisi na maafisa usalama wa nchi hiyo kuwakandamiza waandamanaji. Kadhalika Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amezungumzia kadhia ya kutumwa na Iran meli za mafuta kwenda Venezuela licha ya vitisho vya Marekani na kuongeza kuwa, madai kwamba Marekani ni nchi yenye nguvu na kutoa vitisho vya kuibua vita, ugaidi na vikwazo, vyote hivyo vimebatilishwa na kuingia meli za Iran katika eneo la Caribbean. Hivi karibuni Iran na katika kuiunga mkono serikali na taifa la Venezuela ambalo limekumbwa na vikwazo na mzingiro wa kiuchumi wa Marekani, ilituma meli tano zilizobeba mafuta kwenda nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Maoni