Jun 02, 2020 11:30 UTC
  • Raisi: Mahakama za kimataifa ziwafuatilie na kuwapandisha kizimbani viongozi watenda jinai wa Marekani

Mkuu wa Chombo cha Mahakama nchini Iran amesema kuwa, viongozi wa Marekani ni watuhumiwa wa kuvunja haki za kimsingi kabisa za binadamu na inabidi wapandishwe kizimbani kwenye mahakama za kimataifa.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo Jumanne hapa mjini Tehran na huku akigusia machafuko yanayoendelea katika kona zote za Marekani amesema, ukatili uliofanywa na jeshi la polisi la Marekani dhidi ya Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika, ndiyo picha halisi ya Marekani.

Mkuu huyo wa Vyombo vya Mahakama vya Iran pia amesema, wale wanaodai ni watetezi wa haki za binadamu wamenyamaza kimya mbele ya ukandamizaji wa haki za kimsingi kabisa za kibinadamu duniani na kuongeza kuwa, suala hapa haliwahusu Wamarekani wasio wazungu tu, bali ubaguzi wa rangi ni kitu kilichokita mizizi nchini Marekani.

Trump na Netanyahu wanachutumiwa kwa kufanya jinai za kivita

 

Jumatatu iliyopita, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani alimuua kikatili Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani.

Sasa badala ya rais wa Marekani kutafakari namna ya kutatua tatizo hilo, ametoa vitisho dhidi ya waandamanaji. Mapema siku ya Ijumaa, Donald Trump aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kuwataja waandamanaji wanaolalamikia mauaji ya Mmarekani mweusi kuwa ni magenge ya wahuni na wahalifu. Si hayo tu lakini vile vile ametangaza serikali ya kijeshi na kutishia kuwapiga risasi waandamanaji. Katika sehemu moja ya ujumbe wake aliandika: "Pamoja na matatizo yote yaliyopo hivi sasa, tutaweza kudhibiti hali ya mambo. Iwapo uasi na uporaji wa maduka utaanza, wafanya fujo watafyatuliwa risasi."

Tags

Maoni