Jun 22, 2020 07:47 UTC
  • Meli ya chakula ya Iran yafika kwenye eneo la majini la Venezuela licha ya vikwazo vya Marekani

Meli ya Iran yenye chakula kwa ajili ya wananchi wa Venezuela imefika kwenye eneo la majini la nchi hiyo ya Amerika ya Latini licha ya Marekani kuiwekea vikwazo nchi hiyo na kuifungia njia zote. Hadi tunapokea habari hii, meli hiyo ilikuwa imekaribia kufika kwenye bandari ya Guaira.

Hujjatullah Sultani, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Caracas ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba meli hiyo ya Iran ambayo imebeba chakula na vifaa vya kupambana na ugonjwa wa corona kwa ajili ya wananchi wa Venezuela, imeshaingia kwenye eneo la majini la nchi hiyo. 

Meli hiyo inayopeperusha bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iliondoka katika bandarini mjini Bandar Abbas kusini mwa Iran tarehe 15 Mei na kuelekea Venezuela.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Meli hiyo yenye jina la Golsan inamilikiwa na Shirika la Meli la Mosakhar Darya na imewasili nchini Venezuela baada ya meli nyingine tano za mafuta za Iran kuvunja vikwazo vya Marekani na kuifikishia mafuta Venezuela bila ya kujali vitisho vilivyotolewa na Marekani.

Baada ya Iran kuipelekea Venezuela meli hizo tano za mafuta, serikali ya Caracas imesema imeweka utaratibu na mfumo maalumu wa kugawa mafuta kote nchini humo. 

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameishukuru sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa karibuni hivi atatembelea Tehran kwa ajili ya kuonana na kuzungumza na viongozi wa Iran na kufuatilia makubaliano ya nchi mbili hasa katika nyuga za nishati, kilimo, fedha, teknolojia, sayansi na masuala ya tiba. 

Tags

Maoni